MWANAFUNZI wa Chuo cha VETA Tanga , Maria Moshi akizungumza na wananchi waliotembelea Banda la VETA kwenye ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga waliotaka kujua mashine ya kutoteleshea vifaranga.

Na Mwandishi Wetu, Tanga
CHUO cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Tanga kimebuni mashine ya kutotoleshea vifaranga yenye uwezo wa kutotolesha vifaranga 840 kwa wakati mmoja, huku mabaki ya maganda ya mayai yakitumika kutengeneza chakula cha kuku.
Akizungumza katika Banda la VETA kwenye Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, mwanafunzi wa chuo hicho, Maria Moshi, amesema mashine hiyo inatoa fursa kwa wafugaji na wajasiriamali kupata vifaranga bora na kuendeleza biashara ya kuku.
Amesema mashine hiyo inaambatana na mashine ya kupima na kuchambua mayai kabla ya kuingizwa kwenye mashine ya kutotoleshea, ambapo mayai yasiyofaa hutenganishwa.
Maria amesema mabaki ya maganda ya mayai yanaweza kuchanganywa na virutubisho na kusagwa ili kuzalisha chakula kingine kinachoweza kutumika katika ufugaji wa kuku.
“Kwa mtu anayefanya biashara ya kuku, mashine hii inampa uhakika wa kupata vifaranga vyenye ubora na baadaye kuwauza au kuendeleza ufugaji,” amesema Maria.
Amesema mashine ya kutotoleshea pamoja na mashine saidizi zinauzwa kwa Sh milioni tatu, huku Chuo kikiwa tayari kuzalisha mashine hizo kulingana na mahitaji ya wateja.


No comments:
Post a Comment