HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 22, 2026

NBAA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA VYUO KATIKA KUENDELEZA ELIMU YA UHASIBU

BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao sambamba na mafunzo ya ana kwa ana kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka vyuo vikuu na vyuo vya kati, kwa lengo la kujadili masuala yanayoibuka katika elimu ya Uhasibu, matumizi ya teknolojia, utoaji wa taarifa endelevu (Sustainability Reporting), masuala ya Utafiti pamoja na maendeleo ya kitaaluma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi, amewashukuru wakufunzi kutoka vyuo mbalimbali kwa mchango wao katika kuwajengea wanafunzi msingi imara wa Taaluma ya Uhasibu na kuwaandaa kufanya vizuri katika mitihani ya Bodi.

Amesema maandalizi mazuri ya wanafunzi kuanzia ngazi za vyuo yana mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wao wanapofikia hatua ya kufanya mitihani ya Bodi.

“Tunaamini wanafunzi wakiandaliwa vizuri katika ngazi za chini, inatusaidia sana sisi kama Bodi kuweza kuanzia sehemu nzuri katika ngazi ya mitihani ya Bodi. Tunawahakikishia kuwa tunatambua mchango wenu na tuko tayari kushirikiana nanyi katika eneo lolote litakalohitajika,” amesema CPA Prof. Siasa I. Mzenzi.

Aidha, amesema Taaluma ya Uhasibu imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na miongozo na viwango vya kimataifa pamoja na mabadiliko ya ndani, hivyo amewataka wakufunzi kuendelea kufuatilia na kufundisha kwa kuzingatia wakati katika mitaala na viwango vya Taaluma, ili kuwawezesha wanafunzi kupata uelewa sahihi na kuondoa mkanganyiko wanapofanya mitihani ya Bodi.

Prof. Mzenzi pia amesisitiza umuhimu wa vyuo kuimarisha maeneo matatu muhimu ambayo ni ufundishaji, utafiti na ushauri wa kitaalamu, akibainisha kuwa utafiti ni eneo ambalo linahitaji kupewa kipaumbele zaidi katika Taaluma ya Uhasibu nchini.

Amesema NBAA iko tayari kushirikiana na vyuo katika kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuendeleza Taaluma hiyo, huku akibainisha kuwa Bodi tayari imepitisha Sera ya Utafiti kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hatua inayolenga kuongeza mchango wa utafiti katika maendeleo ya Taaluma ya Uhasibu.

Amewahimiza viongozi wa vyuo na wakufunzi kutumia fursa hiyo kuimarisha tafiti katika Taaluma ya Uhasibu, akisema tafiti kwenye taaluma hiyo bado ni chache ikilinganishwa na umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi na Taaluma nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha kwa njia ya mtandao sambamba na mafunzo ya ana kwa ana kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati iliyofanyika katika ofisi za NBAA, jijini Dar es Salaam tarehe 21, Agosti 2026.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati.
Mdhibiti Ubora Mwandamizi kutoka NACTVET Dkt. Bonaventure Ackles akitoa mada  wakati wa warsha kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati
Mfanyakazi wa NBAA Mike Mangushi akiwasilisha mada kuhusu utoaji wa taarifa endelevu (Sustainability Reporting) kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati
Mfanyakazi wa NBAA CPA Simon Mangesho akitoa mada kuhusu mbinu bora za kufundisha na kufundisha kikamilifu maudhui ya mitaala ya kitaaluma kwa kutumia mfano wa B2 na C1kwa Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati.
Baadhi ya Wafanyakazi wa NBAA na Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati
wakifuatilia mada pamoja na wale wanaofuatilia kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa I. Mzenzi (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NBAA pamoja Wakuu wa Idara za Uhasibu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad