Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BARAZA la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema Maonesho ya Kilimo na Mifugo ya Nane Nane ni fursa muhimu ya kutoa elimu kwa wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya kati vinavyotoa mafunzo katika fani za kilimo na mifugo kuhusu fursa za kujiajiri katika sekta hizo.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo na Mifugo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, jijini Dodoma, Afisa Udhibiti Ubora wa NACTVET, Doris Chiwambo, amesema sekta ya kilimo ina fursa kubwa za ajira na kujiajiri, hivyo wahitimu wa fani za kilimo na mifugo wanapaswa kutumia ujuzi walioupata kuanzisha shughuli za uzalishaji.
Amesema wahitimu hao wanaweza kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na utoaji wa elimu na huduma za kitaalamu katika sekta hizo.
“Sekta ya kilimo ina fursa nyingi za ajira na kujiajiri. Wahitimu wa fani za kilimo na mifugo wanaweza kutumia elimu na ujuzi walioupata kujiajiri katika kilimo, ufugaji na hata kutoa elimu kwa jamii,” amesema Chiwambo.
Aidha, amesema maonesho hayo ni fursa pia kwa wananchi wanaopanga kuanzisha vyuo vinavyotoa mafunzo ya kilimo, mifugo na uvuvi kupata elimu na maelekezo kuhusu taratibu na vigezo vya kuanzisha na kuendesha vyuo hivyo.
Chiwambo amesema NACTVET itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, pamoja na kuhakikisha jamii inaelewa huduma zinazotolewa na baraza hilo ili kufanikisha lengo la kutoa elimu na mafunzo yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Ameongeza kuwa ushiriki wa NACTVET katika maonesho hayo unalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na fursa zinazopatikana kupitia taaluma za kilimo, mifugo na uvuvi.


.jpeg)
No comments:
Post a Comment