HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 6, 2026

Kikwete: Afrika Ikikosa Kuwekeza kwa Vijana Itapitwa na Ajira Milioni 250 za Kidijitali

 



Na Avila Kakingo
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema Afrika inaweza kukosa kunufaika na ajira milioni 250 zinazotarajiwa kuzalishwa na uchumi wa kidijitali duniani iwapo haitawekeza katika kuwajengea vijana ujuzi wa teknolojia za kisasa, hususan Akili Mnemba (Artificial Intelligence–AI).

Akizungumza katika Jukwaa la Miundombinu Afrika lililofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 jijini Dar es Salaam, leo Agosti 06, 2026 Dkt. Kikwete amesema mustakabali wa ajira duniani unategemea zaidi uwezo wa watu kumiliki ujuzi wa kidijitali.

"Kutakuwa na ajira milioni 250 za kidijitali, lakini zitapatikana kwa watu wenye ujuzi. Tusipowekeza katika elimu na kuwajengea vijana wetu uwezo huo, hatutaweza kuzipata fursa hizo."

Pia amesema dunia imehama kutoka kwenye mjadala wa upatikanaji wa intaneti na sasa inaingia katika enzi ya Akili Mnemba, teknolojia ambayo inaendelea kubadili namna ya uzalishaji, utoaji wa huduma na ukuaji wa uchumi.

"Leo hii habari kubwa duniani ni Artificial Intelligence. Hatuwezi kubaki kwenye matumizi ya kawaida ya intaneti wakati dunia imekwenda hatua nyingine. Lazima nasi tujiandae kuitumia teknolojia hiyo kusukuma maendeleo yetu," amesema.

Dkt. Kikwete amesema AI inaweza kuwa chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, afya, uhandisi, elimu na maeneo mengine ya uzalishaji, endapo mataifa ya Afrika yatawekeza katika elimu, utafiti na ubunifu.

Aidha, amesisitiza kuwa mageuzi ya kidijitali yanapaswa kuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya miundombinu ya Afrika, akieleza kuwa bara hilo linapaswa kujiandaa kwa uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia.

Vilevile, amekumbusha kuwa viongozi wa Afrika walikubaliana kupitia Dira ya Afrika 2063 kujenga bara lenye maendeleo jumuishi na miundombinu ya kisasa, huku taasisi ya Africa50 ikiwa miongoni mwa vyombo vinavyoongoza juhudi za kuharakisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya miundombinu.

Dkt. Kikwete amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu unaowakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji na wadau wa maendeleo kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu na uchumi wa bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad