HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 11, 2026

Hospitali ya SINO Yaipa Nguvu Tanzania Katika Utalii Tiba




Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameanza kunufaika na huduma za matibabu ya kibingwa zinazopatikana nchini, hali inayopunguza gharama na ulazima wa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Universal Medical Tourism, Dkt. Sharif Mollel, amesema huduma hizo zinapatikana katika Hospitali ya SINO iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam.

Amesema kampuni yake inashirikiana na hospitali hiyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa, teknolojia za kisasa za matibabu pamoja na baadhi ya huduma za tiba za jadi za China, zinazojulikana kama Traditional Chinese Medicine. Amesema uwepo wa huduma hizo nchini unawapa Watanzania nafasi ya kupata matibabu bila kuingia gharama za tiketi za ndege, malazi, visa na matumizi mengine yanayotokana na safari za matibabu nje ya nchi.

“Lengo letu ni kuona Watanzania wanapata huduma nyingi zaidi hapa nchini. Kama huduma inayohitajika inapatikana Tanzania, hakuna sababu ya mgonjwa kuanza na safari ya kwenda nje ya nchi,” amesema.

Amesema baadhi ya wagonjwa kutoka nchi za Afrika Mashariki na ukanda wa SADC pia wameanza kuja Tanzania kupata huduma katika hospitali hiyo. Kwa mujibu wa Dkt. Mollel, hatua hiyo inaonesha kuwa Tanzania ina nafasi ya kujijenga kuwa kituo muhimu cha huduma za afya na medical tourism katika ukanda wa Afrika.

“Tunataka kuona medical tourism ikienda pande zote. Siyo Watanzania kwenda nje kutibiwa pekee, bali pia wagonjwa kutoka nchi nyingine kuja Tanzania kupata huduma,” amesema.

Amesema Hospitali ya SINO inatoa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu kwa kutumia teknolojia za kisasa, zikiwemo huduma za mifupa na viungo, mgongo, mfumo wa neva, urology na physiotherapy. Hospitali hiyo pia ina teknolojia za uchunguzi zikiwemo Ultrasound, CT Scan na MRI, zinazosaidia madaktari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuamua aina ya matibabu anayohitaji mgonjwa.

Mbali na tiba za kisasa, amesema Hospitali ya SINO inatoa baadhi ya huduma za Traditional Chinese Medicine, ikiwemo acupuncture, inayotumia sindano maalumu katika maeneo mahususi ya mwili chini ya usimamizi wa wataalamu. Amesema huduma hizo zinaweza kusaidia katika usimamizi wa baadhi ya hali za maumivu, misuli na viungo baada ya mgonjwa kufanyiwa tathmini ya kitaalamu.

Dkt. Mollel amesisitiza kuwa huduma za tiba za jadi za China hazikusudii kuchukua nafasi ya tiba za kisasa, bali hutolewa kulingana na ushauri na tathmini ya wataalamu. Ametoa wito kwa Watanzania, hususan wakazi wa Dar es Salaam, kutumia nafasi ya kuwepo kwa huduma hizo nchini kabla ya kufanya uamuzi wa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.

Dkt. Mollel amesema moja ya malengo ya Universal Medical Tourism ni kuendelea kuvutia wataalamu, teknolojia na uwekezaji wa afya kutoka nje ya nchi ili huduma nyingi zaidi zipatikane Tanzania. Amesema kampuni hiyo pia inalenga kuendeleza ushirikiano kati ya madaktari wa Tanzania na wataalamu kutoka China kupitia kambi za matibabu na programu mbalimbali za kubadilishana ujuzi.

“Tunapotengeneza mazingira ya daktari wa Tanzania kufanya kazi pamoja na mtaalamu kutoka China, tunamhudumia mgonjwa lakini pia tunajenga uwezo wa wataalamu wetu,” amesema. Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia teknolojia na maarifa yanayoletwa nchini kubaki na kutumika kwa muda mrefu badala ya huduma kutegemea wataalamu wa nje pekee.

Dkt. Mollel amesema dhamira ya muda mrefu ni kuona Tanzania inapunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kusafiri nje kwa huduma zinazoweza kutolewa nchini, huku ikiongeza idadi ya wagonjwa kutoka mataifa mengine wanaokuja kupata matibabu hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad