HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 11, 2026

GEL yawafungulia milango fursa za elimu duniani wanafunzi 387

 

Na Mwandishi Wetu.
GLOBAL Education Link (GEL) imewakabidhi nyaraka rasmi za safari wanafunzi 387 wa Kitanzania wanaotarajia kwenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu nchini China na India, huku wakihimizwa kutumia fursa hiyo kujenga maarifa, ujuzi, teknolojia, mitandao ya kimataifa na uwezo wa kujitengenezea fursa za maisha, badala ya kulenga shahada pekee.

Ukabidhi huo umefanyika kupitia mikutano miwili maalumu iliyofanyika Agosti 10 na 11, 2026 katika Ukumbi Mkuu wa Makao Makuu ya Global Education Link, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wazazi pamoja na walezi wa wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 198 wanaelekea China na 189 India kwa ajili ya kuanza masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Lengo la mikutano hiyo lilikuwa kuwakabidhi wanafunzi nyaraka muhimu za safari zilizokamilishwa na GEL, zikiwemo pasipoti, visa, tiketi za ndege, NOC (No Objection Certificate), cheti au kijitabu cha chanjo ya homa ya manjano (Yellow Fever Certificate) pamoja na nyaraka nyingine zinazohitajika na mamlaka husika kulingana na nchi, chuo na masharti ya safari.

Mbali na kukabidhiwa nyaraka hizo, wanafunzi pamoja na wazazi na walezi wao walipata maelekezo ya mwisho kuhusu taratibu za safari, uhamiaji, mazingira ya vyuo, makazi, bima ya afya, usalama, matumizi ya fedha, nidhamu na namna ya kukabiliana na mazingira mapya watakapofika katika nchi wanazokwenda.

Mtoa mada mkuu katika mikutano hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, akishirikiana na wawakilishi wa vyuo kutoka China na India waliotoa ufafanuzi kuhusu masomo, huduma za vyuo na maisha ya mwanafunzi wa kimataifa.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mollel aliwataka wanafunzi kutokwenda China na India kwa lengo la kupata cheti au shahada pekee, bali kutumia mazingira ya vyuo watakakosoma kujenga uwezo mpana utakaowasaidia baada ya kuhitimu.

Alisema kwenda kusoma nje ya nchi kunamfungulia mwanafunzi mazingira mapya yenye teknolojia, maabara, warsha, vituo vya ubunifu, wataalamu pamoja na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni jukumu la mwanafunzi kutumia fursa hizo kwa manufaa yake na Taifa.

Aliwataka vijana hao kwenda zaidi ya masomo ya darasani kwa kutembelea maabara, warsha na vituo vya ubunifu na kujifunza kwa vitendo namna teknolojia na bidhaa mbalimbali zinavyozalishwa na kutumika katika kutatua changamoto za jamii.

Akitolea mfano mwanafunzi anayesomea Business Administration, alisema haipaswi kutosha kujifunza nadharia za usimamizi wa biashara pekee, bali anapaswa kutafuta maarifa kuhusu bidhaa, teknolojia, uzalishaji na mifumo mbalimbali ya viwanda ili aweze kuelewa kile anachoweza kukisimamia au kukigeuza kuwa biashara.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad