HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 17, 2026

Airtel Money School Pay Yarahisisha Ulipaji Ada, Shule Zaidi ya 800 Zajiunga Tanzania.

 


HUDUMA  ya Airtel Money School Pay imeendelea kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa ada za wanafunzi nchini, huku shule zaidi ya 800 kutoka mikoa 16 zikiwa tayari zimejiunga na kutumia mfumo huo wa kidigitali unaolenga kurahisisha malipo kwa wazazi na uendeshaji wa kifedha kwa shule.

Akizungumza wakati wa ziara katika Salaam Pre and Primary School, iliyopo Chamazi, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Afisa Huduma wa Airtel Money School Pay, Roda William Mganga, alisema huduma hiyo ilianzishwa mwaka 2024 ikiwa na lengo la kutoa njia rahisi, salama na yenye ufanisi katika ulipaji wa ada na usimamizi wa taarifa za malipo.

Mganga alisema tangu kuanzishwa kwake, School Pay imefanikiwa kufikia shule zaidi ya 800 katika mikoa 16 nchini, huku lengo likiwa ni kuunganisha shule 1,000 kila mwaka. Mikoa ambayo tayari imefikiwa na huduma hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Arusha, Mwanza na Mtwara.

Alisema miongoni mwa shule zinazotumia mfumo huo ni pamoja na St. Anne Maria Academy, Fountain Gate Schools, St. Anthony’s Secondary School, Salaam Pre and Primary School, Living Minds Pre and Primary School, Memon Pre and Primary School na Mbwawa Lutheran Secondary School, huku Airtel pia ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kidini zinazoendesha shule.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Salaam Pre and Primary School, Kalunji Mkasa Idris, alisema shule hiyo imekuwa ikitumia School Pay tangu Septemba mwaka jana na kwamba mfumo huo umeleta mabadiliko makubwa katika ukusanyaji na usimamizi wa ada.

Alisema awali shule ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za kupokea fedha taslimu, jambo ambalo liliongeza hatari ya fedha kupotea na kufanya ufuatiliaji wa malipo kuwa mgumu.

“School Pay imetusaidia sana katika ukusanyaji wa ada. Sasa fedha zinazoingizwa kupitia mfumo zinaonekana na kuingia benki, hivyo tunapata kumbukumbu sahihi na tunakuwa na uwezo wa kuzitumia kwa mahitaji ya shule,” alisema Idris.

Aidha, alisema mfumo huo umewarahisishia wazazi kwa kuwa hawalazimiki tena kwenda benki na kusimama kwenye foleni ili kulipia ada. Kwa mujibu wake, mzazi anaweza kufanya malipo kupitia simu yake wakati wowote, ikiwemo nyakati za usiku, na taarifa ya malipo kuonekana kwenye mfumo wa shule ndani ya muda mfupi, hivyo kurahisisha utoaji wa risiti na ufuatiliaji wa malipo.

Mhasibu wa Salaam Pre and Primary School, Fatma Yusuf, alisema School Pay imekuwa na mchango mkubwa katika kuweka kumbukumbu sahihi za malipo ya ada na kuwawezesha wazazi kupata risiti mara baada ya kufanya malipo.

Alisema mfumo huo umepunguza ulazima wa wazazi kufika shuleni kwa ajili ya kufanya malipo au kufuatilia risiti, kwani wanaweza kukamilisha mchakato huo wakiwa nyumbani.

Naye mzazi wa mwanafunzi wa Salaam Pre and Primary School, Hassan Said Malipa, alisema mfumo huo umemsaidia yeye na wazazi wengine kufuatilia kwa urahisi kiasi cha ada kilicholipwa na salio lililobaki. Alisema uwezo wa kufanya malipo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa kipato umekuwa msaada mkubwa kwa wazazi, huku taarifa za malipo zikipatikana kwa wakati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad