HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 22, 2026

Absa Tanzania Yaongeza Juhudi za Kuwawezesha Wasichana katika Teknolojia kupitia GirlCode Hackathon

 Benki ya Absa Tanzania, kwa kushirikiana na GirlCode, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake nchini Afrika Kusini linalolenga kuwawezesha wasichana kutoka mazingira yenye changamoto kwa kuwapatia ujuzi na rasilimali za kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta ya teknolojia, imetangaza kurejea kwa mashindano ya GirlCode Tanzania Hackathon kwa mwaka wa pili mfululizo.

Hatua hiyo inafuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka 2025, ambapo timu ya Tanzania iliibuka na tuzo kuu ya Pan-African Grand Prize yenye thamani ya Dola za Marekani 5,000.

GirlCode Hackathon ni sehemu ya mpango mpana wa GirlCode unaolenga kuwawezesha wanawake vijana barani Afrika kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo katika teknolojia, kuwaunganisha na walezi na wataalamu kupitia programu za ushauri, pamoja na kuwapa fursa ya kubuni suluhisho zinazolenga kukabiliana na changamoto halisi katika jamii zao.

Kurudi kwa mashindano hayo nchini Tanzania kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha kizazi cha wataalamu wanawake katika teknolojia na kujenga juu ya mafanikio yaliyopatikana na washiriki wa Tanzania mwaka jana.

Ushindi wa Tanzania mwaka 2025 ulidhihirisha umuhimu wa kuwekeza kwa wanawake vijana kama wabunifu, wajenzi wa suluhisho na watatuzi wa changamoto. Mafanikio hayo hayakuweka tu Tanzania katika ramani ya GirlCode Hackathon barani Afrika, bali pia yalitoa hamasa kwa wanawake vijana zaidi nchini kujiona kuwa sehemu ya uchumi wa kidijitali unaokua barani Afrika.

Akizungumzia kurejea kwa mpango huo nchini Tanzania, Ofisa Mtendaji Mkuu wa GirlCode, Zandile Mkwanazi, alisema shirika hilo linajivunia mafanikio yaliyopatikana na timu ya Tanzania mwaka jana.

“GirlCode inajivunia sana kile ambacho timu ya Tanzania ilifanikiwa kukipata mwaka jana. Kushinda tuzo kuu ya Pan-African Grand Prize kumeonyesha kiwango cha vipaji, ubunifu na uwezo uliopo miongoni mwa wanawake vijana nchini Tanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa kurejea kwa mashindano hayo kwa mwaka wa pili kunalenga kujenga juu ya mafanikio yaliyopatikana na kuwapa wanawake vijana zaidi fursa ya kuendeleza ujuzi wao, kufanya kazi kwa pamoja na kubuni suluhisho zinazotumia teknolojia na ambazo zinaweza kuwa na matokeo chanya katika jamii.

Hackathon ya mwaka huu itawakutanisha wanafunzi wa kike, wahitimu, wanaotarajia kuwa watengenezaji wa programu pamoja na wabunifu vijana, ambao watashirikiana katika timu, kupata ushauri kutoka kwa wataalamu na kuwasilisha suluhisho zao mbele ya jopo la majaji.

Washiriki watatakiwa kutumia fikra tunduizi, kutumia ujuzi wao wa kiteknolojia na kubuni mawazo mapya yanayoweza kuchangia katika mustakabali wa ajira, ujasiriamali na mageuzi ya kidijitali.

Mbali na mashindano, mpango huo utatoa jukwaa muhimu kwa wanawake vijana kupata uzoefu na uelewa zaidi kuhusu sekta ya teknolojia, kuunganishwa na wenzao pamoja na washauri, na kujenga kujiamini katika kutafuta ajira na fursa mbalimbali katika sekta hiyo.

Kwa washiriki wengi, uzoefu huo unaweza kuwa hatua ya kuingia katika programu za mafunzo kwa vitendo, ajira, ujasiriamali na kuendelea kujifunza katika teknolojia.

Akizungumzia umuhimu wa mpango huo, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Absa Tanzania, Oscar Mwamfwagasi, alisema ushiriki wa waanzilishi wa biashara ndogo na za kati (SMEs) ni moja ya mambo yanayoongeza thamani katika Hackathon ya mwaka huu.

“Kinachofanya Hackathon ya mwaka huu kuwa na thamani zaidi ni ushiriki wa moja kwa moja wa waanzilishi wa biashara ndogo na za kati, ambao wanaleta uzoefu wa vitendo katika biashara pamoja na changamoto halisi zinazokabili biashara kwenye programu hii.”

Alisema ushiriki wao unasaidia kuboresha safari ya kujifunza kwa washiriki, huku ukifungua fursa kwa kampuni changa kuonyesha mawazo yao, kupata mwongozo kutoka kwa wataalamu wa sekta mbalimbali na kujenga mahusiano yanayoweza kusaidia kuharakisha ukuaji wa biashara zao.

“Programu kama hii ni muhimu katika kukuza ubunifu, kuwawezesha wajasiriamali na kujenga mfumo jumuishi zaidi wa kidijitali unaosaidia maendeleo endelevu ya Afrika,” alisema Mwamfwagasi.

Kadiri GirlCode Hackathon inavyoendelea kukua katika mataifa mbalimbali ya Afrika, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kile kinachoweza kufikiwa pale wanawake vijana wanapopewa majukwaa, rasilimali na mitandao sahihi ya kuwawezesha.

Ushindi wa Tanzania katika mashindano ya Pan-African mwaka 2025 umeweka msingi imara, huku toleo la mwaka huu likilenga kutoa hamasa kwa kizazi kijacho cha wanawake wa Tanzania wanaotaka kujikita katika teknolojia kufikia mafanikio makubwa zaidi.

GirlCode imewahimiza wanawake vijana nchini Tanzania, wadau, walezi na washiriki wa mfumo wa teknolojia kuunga mkono Hackathon ya mwaka huu na kushirikiana katika kujenga mustakabali wa kidijitali unaojumuisha watu wengi zaidi barani Afrika.

GirlCode Tanzania Hackathon 2026 itafanyika tarehe 26–27 Septemba 2026.

Maombi ya ushiriki: https://www.girlcode.co.za/hackathon-2026


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad