Msimamizi wa duara katika Mgodi wa Uchimbaji wa Madini wa Mwabageni uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Sengerema Gambo, anatuhumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kujiunganishia huduma ya umeme kinyume na taratibu za shirika hilo.
Kiongozi wa Operesheni ya Kubaini na Kuwakamata Wateja Wanaoharibu Miundombinu ya TANESCO Mkoa wa Geita, ambaye pia ni Mkuu wa Usalama wa TANESCO Mkoa huo, Eleutherius Katemana, amewataka wateja wote wa umeme kufuata taratibu rasmi za kuunganishiwa huduma hiyo ili kuepuka kuvunja sheria na kuhatarisha usalama wa miundombinu ya umeme.
Katemana amesema mtuhumiwa alitumia nguzo na nyaya za TANESCO kwa kushirikiana na mkandarasi wake bila kufuata taratibu zinazotakiwa na shirika hilo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za utoaji wa huduma ya umeme.
Kwa upande wake, Sengerema Gambo amekanusha tuhuma hizo akidai kuwa alifuata taratibu zote zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kufanya manunuzi ya vifaa vinavyohitajika na kumuita mkandarasi wake kufunga miundombinu hiyo.
Aidha, Katemana amewatahadharisha wananchi na wateja wa TANESCO mkoani Geita kuacha kutumia wakandarasi wanaokiuka taratibu za shirika hilo. Amesema badala yake wanapaswa kufika katika ofisi za TANESCO kupata ushauri na kufuata utaratibu rasmi wa kuunganishiwa umeme.
Ameongeza kuwa vitendo vya kuunganisha umeme kinyume na utaratibu vinaihujumu TANESCO kwa kuisababishia hasara ya mapato, kuharibu miundombinu ya umeme na vifaa vya wateja, huku lawama nyingi zikiielekezwa kwa shirika hilo badala ya wahusika halisi.





No comments:
Post a Comment