HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 3, 2026

WAHASIBU TARURA WAPEWA MAFUNZO KUONGEZA UFANISI


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imefungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), yanayofanyika katika Hoteli ya KingsWay mkoani Morogoro, kwa lengo la kuimarisha taaluma ya uhasibu na kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi.

‎Akifungua mafunzo hayo rasmi Julai 9, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi, ameipongeza TARURA kwa kuthamini mchango wa wahasibu na kuitaja kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine za umma katika kuendeleza taaluma hiyo.

‎Amesema katika baadhi ya taasisi wahasibu bado hawaonekani kama sehemu muhimu ya maamuzi ya kimkakati, bali hupewa nafasi zaidi wakati wa ukaguzi wa hesabu, hali ambayo inapaswa kubadilika ili taaluma hiyo iwe chachu ya maendeleo ya taasisi.

‎CPA Prof. Mzenzi amesema NBAA itaendelea kushirikiana kwa karibu na TARURA kwa kutoa msaada wa kitaalamu kila unapohitajika, ili kuhakikisha uhasibu unaongeza thamani katika utekelezaji wa majukumu ya wakala huo.

‎Aidha, amewahimiza wahasibu ambao bado hawajakamilisha mchakato wa kupata sifa za kitaaluma kuendelea na juhudi za kujiendeleza, akieleza kuwa hatua hiyo itawanufaisha binafsi katika maendeleo ya taaluma zao na kuongeza hadhi ya taasisi wanazozitumikia.

‎Pia amesisitiza umuhimu wa TARURA kuzingatia eneo la taarifa za uendelevu (Sustainability Reporting), akibainisha kuwa kutokana na wakala huo kufanya kazi kwa karibu na wakandarasi wa ujenzi wa barabara, una fursa kubwa ya kuwa kinara katika utekelezaji wa mfumo huo.

‎Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa TARURA, CPA Jacob Nyaulingo, amesema wakala huo umefikia hatua za mwisho za kuandaa Sera ya Uwekezaji (Investment Policy), ambayo itaanza kutumika rasmi ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa masuala ya uwekezaji ndani ya Taasisi.
 Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akizungumza na watumishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tatu yanayofanyika mkoani Morogoro
Mhasibu Mkuu wa TARURA, CPA Jacob Nyaulingo akizungumza na viongozi wa NBAA pamoja na watumishi wa TARURA wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya suku tatu kwa watumishi hao.
Mkurugenzi wa Viwango, Utafiti na Huduma za Kiufundi NBAA, CPA Angyelile Tende akitoa mafunzo kwa watumishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) yanayofanyika mkoani Morogoro.
Baadhi ya wahasibu wa TARURA wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi alipokuwa anafungua mafunzo hayo ya siku tatu.
Picha ya pamoja



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad