Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema usimamizi na ufuatiliaji unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) umechangia kwa kiwango kikubwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha za umma (Value for Money).
Shigela amesema hayo wakati wa warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Amesema TAKUKURU Mkoa wa Geita imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kudhibiti mianya ya rushwa, hali iliyochangia kukamilika kwa miradi mingi inayotoa huduma muhimu kwa wananchi katika sekta za afya, maji, elimu na miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, James Ruge, amesema Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ruge amesema mafanikio ya miradi hiyo yanategemea uwepo wa usimamizi madhubuti katika kila hatua ya utekelezaji, ikiwemo upangaji wa miradi, uidhinishaji, utekelezaji, usimamizi wa mikataba na ukaguzi wa utekelezaji wake.
Ameongeza kuwa TAKUKURU itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia utekelezaji wa sheria zinazolinda rasilimali za umma na kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Warsha hiyo imewakutanisha viongozi na watendaji kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Geita, ambapo walipata mafunzo na elimu kuhusu wajibu wao katika usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na umuhimu wa kushirikiana na TAKUKURU ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuleta maendeleo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)

No comments:
Post a Comment