Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi nchini ili kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na utoaji mimba usio salama.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi alisema bungeni kuwa asilimia 10 ya vifo vya wajawazito nchini vinahusishwa na utoaji mimba usio salama, hali inayoonyesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika kinga, elimu na huduma za matibabu kwa wanawake.
Alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeboresha miundombinu ya sekta ya afya na kuendelea kutoa huduma jumuishi baada ya utoaji mimba (CPAC) bila malipo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
"Tunawapatia wanawake huduma baada ya kuharibikiwa na mimba, ikiwemo matibabu, dawa, ushauri nasaha na elimu ya uzazi wa mpango ili kupunguza hatari ya kupata mimba nyingine isiyotarajiwa na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza," alisema Dk Samizi.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuimarisha huduma rafiki kwa vijana kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi, kujikinga dhidi ya mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa, pamoja na kuhakikisha manusura wa ukatili wa kijinsia na matukio mengine wanapata huduma stahiki kwa wakati.
Kauli hiyo imekuja wakati wadau mbalimbali wakiendelea kujadili utekelezaji wa Itifaki ya Maputo, ambayo Tanzania iliiridhia.
Mjadala umejikita zaidi kwenye Ibara ya 14(2)(c) ya itifaki hiyo, inayozitaka nchi wanachama kuchukua hatua zinazofaa kuruhusu utoaji mimba kwa njia ya tiba katika mazingira maalumu, ikiwemo pale ujauzito umetokana na ubakaji, unyanyasaji wa kingono, ndugu wa damu (incest), au endapo kuendelea kwa ujauzito kunaweka maisha au afya ya mama katika hatari, au maisha ya kijusi yako hatarini. Utekelezaji wa masharti hayo unafanyika kwa kuzingatia sheria za ndani za kila nchi.
Nchini Tanzania, utoaji mimba kwa hiari bado unadhibitiwa na sheria, isipokuwa katika mazingira yanayotambuliwa na sheria husika.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa wanawake wanaopata madhara baada ya utoaji mimba wanapaswa kufika katika vituo vya afya ili wapate matibabu, ushauri nasaha na huduma nyingine muhimu bila kuchelewa.
Wataalamu wa afya wanasema utoaji wa huduma hizo, sambamba na elimu ya afya ya uzazi na upatikanaji wa huduma kwa wakati, ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kupunguza vifo vya kina mama na kuboresha afya ya uzazi nchini

.jpeg)

No comments:
Post a Comment