HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 3, 2026

SERIKALI YAKIPONGEZA TPSC KWA MAFANIKIO MAKUBWA YA MIAKA 25 YA KUIMARISHA UTUMISHI WA UMMA.

Dar es Salaam, Julai 3, 2026 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, akisema Chuo kimejidhihirisha kuwa nguzo muhimu ya Serikali katika kujenga watumishi wa umma wenye maarifa, stadi, maadili na uzalendo unaohitajika katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya TPSC yaliyofanyika katika Julius Nyerere International Convention Centre, Kikwete amesema Chuo kimepitia hatua kubwa za maendeleo kwa kupanua huduma zake na kuongeza mchango wake katika kuimarisha utumishi wa umma nchini.

"Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Chuo hiki kimepitia hatua kubwa za maendeleo. Kutoka kampasi mbili wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia kampasi sita leo; kutoka programu chache za mafunzo hadi kuwa taasisi inayotoa mafunzo ya muda mfupi, programu za muda mrefu, mafunzo kwa njia ya mtandao, tafiti tumizi na shauri za kitaalamu. Haya yote ni mafanikio makubwa yanayostahili pongezi za dhati," amesema Kikwete.

Kikwete pia amekipongeza Menejimenti ya Chuo kwa kuimarisha tafiti tumizi, akisema uzinduzi wa tafiti sita wakati wa maadhimisho hayo unaonesha dhamira ya TPSC ya kuwa kitovu cha maarifa na ushahidi wa kisayansi kinachosaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi ya sera, kuboresha mifumo ya kazi na kuongeza ufanisi wa huduma za umma.

Kwa upande wake, Mkuu na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa dhamira ya Chuo ya kuimarisha utumishi wa umma kupitia mafunzo, tafiti na huduma za ushauri wa kitaalamu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.

Aidha Dkt. Mabonesho amesema katika kipindi hicho Chuo kimeongeza idadi ya kampasi kutoka mbili hadi sita, kupanua programu za mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, kuanzisha mafunzo kwa njia ya mtandao na kuimarisha tafiti tumizi pamoja na ushauri wa kitaalamu ili kukidhi mahitaji ya watumishi wa umma nchini.

"Upanuzi huu umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha mafunzo na huduma za kitaalamu," alisema Dkt. Mabonesho.

Pia ameongeza kuwa TPSC itaendelea kuwekeza katika ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuendelea kuwa kitovu cha maendeleo ya rasilimali watu na taasisi inayoongoza katika kujenga utumishi wa umma wenye ufanisi nchini na barani Afrika.















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad