HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 6, 2026

Sekretarieti ya Maadili: Hatuna Ugomvi na Viongozi Matajiri Waliopata Utajiri Halali

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

OFISI ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema haina tatizo na viongozi wa umma wenye utajiri, ilimradi mali walizonazo zimepatikana kwa njia halali bila kutumia vibaya madaraka yao au kufanya biashara zinazokinzana na nafasi wanazoshikilia serikalini.

Hayo ameyasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi hiyo, Honoratus Ishengoma, wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ishengoma alisema viongozi wa umma wanatakiwa kuzingatia masharti ya kimaadili yaliyowekwa na sheria, ikiwemo wajibu wa kutangaza mali na madeni yao pamoja na kueleza vyanzo vya mapato yao ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Amesema kuwa lengo la ushiriki wa Sekretarieti katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya taasisi hiyo, maadili yanayopaswa kuzingatiwa na viongozi wa umma pamoja na umuhimu wa kuzingatia miiko ya uongozi katika utendaji wa kila siku.

Aidha, alisema sheria haiwazuii viongozi wa umma kufanya biashara au shughuli nyingine za kiuchumi, mradi shughuli hizo hazisababishi mgongano wa maslahi na majukumu yao ya kikazi au kutumia nafasi za uongozi kujinufaisha binafsi.

Aliwahimiza wananchi kutembelea banda la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu maadili ya viongozi, wajibu wa viongozi kutangaza mali zao na nafasi ya wananchi katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad