Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali wameagizwa kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unakuwa sehemu ya majukumu yao ya kila siku kwa kuoanisha mipango, bajeti na maamuzi ya Taasisi wanazoziongoza na malengo ya maendeleo ya Taifa.
Agizo hilo limetolewa Julai 24, 2026 Kibaha mkoani Pwani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Watendaji Wakuu yaliyolenga kuimarisha uongozi na utendaji wa Taasisi za Umma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ridhiwani amewakumbusha Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ulianza rasmi Julai Mosi mwaka huu, hivyo wanapaswa kuhakikisha agenda hiyo inaakisiwa katika utekelezaji wa bajeti, vipaumbele na mipango mkakati ya taasisi zao ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayatapatikana kwa matamko pekee, bali kupitia maamuzi ya kila siku yatakayofanywa na viongozi wa Taasisi.
Aidha, amesema kila bajeti, mradi, uwekezaji na huduma inayotolewa inapaswa kuonyesha mchango wake katika kufanikisha malengo ya Dira 2050.
Sambamba na hayo, amewataka kuhakikisha viashiria vya utendaji vya taasisi zao vinaendana moja kwa moja na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kurahisisha upimaji wa mchango wa kila Taasisi katika utekelezaji wa Dira hiyo kila mwaka na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
"Nina imani kuwa maarifa na uzoefu mlioupata utatafsiriwa katika utendaji wenye matokeo chanya, hivyo kuimarisha utawala bora, kuongeza ufanisi wa Taasisi za Umma na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya Taifa," amesema Mhe. Ridhiwani.
Katika kuhitimisha mafunzo hayo, Mhe. Ridhiwani aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina, Taasisi ya Uongozi na wadau kwa maandalizi na uratibu wa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewajengea uwezo wa kuongoza Taasisi kwa ufanisi, kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali..jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment