
Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2026.
Na Mwandishi Wetu
WAKATI uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China ukiendelea kuimarika, Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji, amesema tathmini ya ushiriki wa Ubalozi wa Tanzania katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) imeibua mkakati wa kuwasaidia Watanzania kutumia fursa za biashara na uwekezaji katika soko la China.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Julai 14, 2026, Dkt. Haji alisema takribani Watanzania 500 walitembelea banda la ubalozi huo na kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wanaotaka kufanya biashara za kimataifa.
Alisema changamoto hizo ni pamoja na uzalishaji hafifu usiokidhi viwango vya kimataifa, uelewa mdogo wa taratibu za biashara za kimataifa, pamoja na udhaifu wa vifungashio unaopunguza ushindani na thamani ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje.
Aidha, alisema wafanyabiashara wengi walieleza kuwa baadhi ya taasisi zinazopaswa kuwawezesha kushiriki katika biashara za kimataifa zimekuwa zikikwamisha juhudi zao badala ya kuzisaidia.
Dkt. Haji alisema Tanzania ina fursa kubwa za kushirikiana na China katika sekta za kilimo, uvuvi, nishati na madini, huku akibainisha kuwa idadi ya watalii kutoka China wanaotembelea Tanzania imefikia takribani 82,000 na inatarajiwa kufikia 100,000 mwaka ujao.
Kutokana na changamoto zilizobainika, alipendekeza kuanzishwa kwa Kliniki ya Biashara itakayotoa elimu na ushauri kuhusu biashara za kimataifa, kuboreshwa kwa utekelezaji wa sera ya ushuru sifuri, kuimarishwa kwa elimu kuhusu fursa zilizopo China na masoko mengine, pamoja na kuanzishwa kwa kituo kimoja kitakachounganisha taasisi zote zinazoshughulikia biashara za kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, alimpongeza Dk. Haji kwa kuanzisha zoezi hilo, akisema litakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika biashara za kimataifa na kuvutia uwekezaji nchini.




.jpeg)
No comments:
Post a Comment