HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 1, 2026

Mhitimu wa Chuo Kikuu Ajiajiri Baada ya Mafunzo ya VETA, Abuni Mavazi kwa Maganda ya Parachichi, Vitunguu na Madafu



Antonia Nsimbi akionesha Shati alilotengeneza kwa kutuma Maganda ya Parachichi.
Antonia Nsimbi akionesha Shati alilotengeneza kwa kutuma Maganda ya Vitunguu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MHITIMU wa Chuo Kikuu cha Saint Augustine cha Mwanza, Antonia Nsimbi, amefanikiwa kujiajiri baada ya kupata mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), ambapo sasa anatengeneza mavazi ya ubunifu kwa kutumia maganda ya parachichi, vitunguu na madafu kama malighafi.

Akizungumza katika banda la VETA kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, Antonia alisema baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu alikaa kwa muda akisaka ajira bila mafanikio, jambo lililomsukuma kutafuta ujuzi wa kujiajiri kupitia VETA.

Alisema mafunzo aliyoyapata yalimwezesha kubuni teknolojia ya kuchakata maganda ya parachichi, vitunguu na madafu na kuyatumia kutengeneza mavazi ya kipekee ambayo kwa sasa yanapata soko kutokana na ubunifu wake na matumizi ya malighafi rafiki kwa mazingira.

"Nilipoanza haikuwa rahisi, lakini kwa sasa naona matunda ya ubunifu huu. Wateja wanapenda bidhaa hizi kwa sababu ni tofauti na zinatengenezwa kwa kutumia malighafi ambazo wengi hawakudhani zinaweza kutumika kutengeneza mavazi," alisema Antonia

Antonia aliwahimiza vijana kuacha kusubiri ajira za kuajiriwa pekee na badala yake kutumia fursa zinazotolewa na VETA kupata ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuanzisha biashara zinazokidhi mahitaji ya soko.

Alisema changamoto ya ajira inaweza kupunguzwa endapo vijana wataamua kuwekeza katika ubunifu na ujuzi wa vitendo, akibainisha kuwa vyuo vya VETA vina mchango mkubwa katika kuwawezesha wahitimu kujenga maisha yao kupitia shughuli za uzalishaji.

Aidha, alieleza kuwa kusubiri ajira serikalini au sekta binafsi kunaweza kuchukua muda mrefu kutokana na idadi kubwa ya wahitaji wa ajira ikilinganishwa na nafasi zinazopatikana, hivyo akasisitiza umuhimu wa kujiajiri kwa kutumia ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo ya ufundi stadi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad