Wapanda Mlima wa kampeni ya GGM HIV Kili Challenge baada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa KIA kwa ajili ya kuanza zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro siku ya Ijumaa
Na Mwandishi Wetu
Shamrashamra na hamasa zimetawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya washiriki wa kampeni ya GGM HIV Kili Challenge kuwasili tayari kwa kuanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kuuzunguka kwa baiskeli, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuchangisha fedha na kuhamasisha mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Safari hiyo rasmi inaanza siku ya Ijumaa, ambapo jumla ya watu 38 watapanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu, huku washiriki wengine 10 wakitarajiwa kuuzunguka mlima huo kwa kutumia baiskeli katika kipindi cha siku saba.
Lengo ni kuhamasisha jamii, taasisi na kampuni mbalimbali kuunga mkono kampeni hiyo kupitia michango itakayosaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za kupambana na VVU na UKIMWI.
Wakizungumza mara baada ya kuwasili kaika uwanja wa KIA, washiriki hao kutoka mkoani Geita walieleza furaha yao kuwa sehemu ya kampeni hiyo na kuahidi kufanya kila jitihada kuhakikisha wanafika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Mmpja wa washiriki hao ambaye tayari amewahi kushiriki mara mbili zilizopita, Bi. Chitegetse Rushatsi alisema ana imani kubwa ya kufanikiwa kufika kileleni tena safari hii .
"Tumepokelewa kwa furaha kubwa na tuna matumaini makubwa ya kufika kileleni. Hii ni mara yangu ya tatu kushiriki, na mara zote nimefanikiwa kufika kileleni. Najivunia kuwa sehemu ya historia hii," alisema.
Kwa upande wake, Bi. Martha Daniel, ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza, alisema kuwa hapo awali alikuwa na hofu, lakini alihamasika baada ya kufahamu umuhimu wa kampeni hiyo.
"Nilipopata taarifa kwamba nimechaguliwa kushiriki nilikuwa na hofu, lakini baada ya kupewa hamasa na kuelezwa umuhimu wa tukio hili niliamua kuwa sehemu ya historia," alisema.
Aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kampeni hiyo, akisema mbali na kusaidia mapambano dhidi ya VVU, pia inachangia kutangaza na kuhamasisha utalii wa ndani.
Bi. Martha pia aliushukuru mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining Limited -GGML) kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wafanyakazi wake kushiriki katika shughuli za kijamii zenye manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla, pamoja na kuipongeza kampuni ya Ahsante Tours kwa kuwa waongozaji wakuu wa safari hiyo.
Katika kuonesha kuwa kampeni hiyo inawahusisha watu wa rika mbalimbali, Marietha Elius, mwanafunzi wa Darasa la Saba mwenye umri wa miaka 13, ni mmoja wa washiriki wa safari hiyo.
Marietha alisema amefurahia kupata nafasi ya kupanda mlima mrefu zaidi barani Afrika huku akichangia jitihada za kuwasaidia watu wanaoishi na VVU.
"Nina furaha mara mbili; kwanza kushiriki kuwasaidia watu wanaohitaji msaada, na pili kupata nafasi ya kuuona na kuupanda Mlima Kilimanjaro ambao wengi wetu tunaujifunza darasani kupitia historia yake," alisema.
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya GGML, Bw.Gilbert Mworia alisema mwitikio wa wadau katika kampeni ya mwaka huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Alisema ongezeko hilo linaonesha dhamira ya wadau mbalimbali kuunga mkono lengo la kufanikisha malengo ya Sifuri Tatu ifikapo mwaka 2030, ambayo inalenga kutokomeza maambukizi mapya ya VVU, kuzuia vifo vinavyotokana na UKIMWI na unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU. Mworia aliongeza kuwa mwaka huu, kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, kampeni hii itaambatana na huduma za upimaji wa VVU na uchangiaji wa damu salama zitakazotolewa katika maeneo mbalimbali ya wananchi, tofauti na miaka iliyopita ambapo huduma hizo zilitolewa katika malango ya Machame na Mweka pekee wakati wa upandaji wa mlima.
Kampeni ya GGM HIV Kili Challenge inaratibiwa na GGML kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) pamoja na wadau mbalimbali. Mbali na kuchangisha fedha kwa ajili ya huduma kwa watu wanaoishi na VVU, kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa jamii, kupunguza unyanyapaa na kusaidia ujenzi wa miundombinu pamoja na huduma nyingine muhimu katika harakati za kutokomeza UKIMWI nchini.


.jpeg)

No comments:
Post a Comment