Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amesema usimamizi madhubuti wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) una mchango mkubwa katika kuwawezesha Watanzania kunufaika na rasilimali za madini, kuongeza vipato vyao na kukuza uchumi wa taifa.
Komba ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Mobile Manufacturing Unit (MMU), mtambo wa kisasa wenye teknolojia ya kuzalisha na kuchaji vilipuzi kwa matumizi ya migodini, unaotarajiwa kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya huduma za vilipuzi migodini.
Amesema uwekezaji wa aina hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya madini, badala ya kutegemea huduma kutoka nje ya nchi.
Mtambo huo wa MMU ni wa kwanza nchini kwa mwekezaji mzawa kuwa nao, ukiwa na uwezo wa kubeba na kuzalisha tani 15 za vilipuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayokidhi mahitaji ya shughuli za uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Geita, Injinia Gasper Kachenge, amesema ujio wa mtambo huo utaongeza mnyororo wa thamani katika sekta ya madini na kufungua fursa zaidi kwa Watanzania kushiriki katika huduma zinazohusiana na uchimbaji wa madini.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo ni ishara ya kukua kwa uwezo wa wazawa katika kuwekeza kwenye teknolojia na huduma zinazohitajika katika sekta ya madini, jambo litakaloongeza tija na thamani ya shughuli za uchimbaji nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ESAP, Injinia Yahya Puyaga, amesema mtambo huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 700 unaonesha uwezo wa Watanzania kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia uwekezaji katika sekta ya madini.
Amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi wa huduma za vilipuzi migodini na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini kupitia sera ya Local Content.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment