.jpeg)
Na Mwandishi Wetu, Temeke
JAMII imetakiwa kuongeza juhudi za kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kukua bila ukatili.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Temeke, Lawama Mikidadi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika wilayani humo.
Mikidadi amesema maadhimisho hayo ni nafasi ya kuikumbusha jamii wajibu wake wa kusimamia ustawi wa watoto.
“Licha ya jitihada zinazofanywa, bado kuna matukio ya ukatili dhidi ya watoto katika baadhi ya maeneo. Ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa,” amesema.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefadhiliwa na taasisi za Boys Initiative Tanzania na Miriam Odemba Foundation, ambazo zimetoa pedi na vifaa mbalimbali kwa watoto 300 walioshiriki.
Kwa upande wake, halmashauri ya Manispaa ya Temeke imadhimisha siku hiyo mapema kabla ya tarehe 16 juni mwaka huu.
Kupitia ushiriki huo, Boys Initiative Tanzania imeendelea kupaza sauti ya mtoto wa kiume, huku Miriam Odemba Foundation ikisimama kutetea na kuwezesha mtoto wa kike, taasisi zote mbili zikifanya kazi ya kuhakikisha watoto wanapata ulinzi, fursa na mazingira bora ya kufikia ndoto zao.
Akizungumza na wanafunzi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Temeke, Brandina Ndunguru, amewataka watoto kuwa makini dhidi ya watu wanaoweza kutumia zawadi au ahadi mbalimbali kuwashawishi.
“Mtoto anapaswa kulindwa, kusikilizwa na kupewa nafasi ya kueleza changamoto zake. Wazazi wajenge urafiki na watoto wao ili waweze kuwasaidia kwa karibu zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Maendeleo ya Mtoto wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Sweetbertha Pascal, amesema halmashauri imeendelea kutoa elimu ya malezi bora na kupinga ukatili wa kijinsia katika shule na mitaa yote 42 ya manispaa hiyo.
Watoto walioshiriki maadhimisho hayo pia wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa haki zao na namna ya kujilinda.
“Sasa tunajua umuhimu wa kutoa taarifa tunapoona au kufanyiwa vitendo visivyofaa ili tupate msaada kwa wakati,” amesema Edwin John kwa niaba ya wanafunzi.
Maadhimisho hayo yalishirikisha shule sita, walimu, viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo ya watoto, yakibeba kaulimbiu isemayo “Mtoto ni Malezi, Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara.”

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment