Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA) zimeanza maandalizi ya Tuzo za Uandishi wa
Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 zikiwa na
lengo la kuendelea kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yenye ubora
yanayochangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza
Jumapili tarehe 31 Mei, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa
mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Mwenyekiti wa SKA, Mha.
Peter Mwasalyanda, amesema SKA ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea
kutambua mchango wa Waandishi wa Habari za maendeleo nchini.
Amesema
tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa
maudhui ya ndani yenye ubora yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na
kuburudisha, huku yakiimarisha taswira chanya ya Taifa kupitia habari za
maendeleo.
Mwasalyanda amesema katika awamu ya kwanza ya tuzo hizo kulikuwa na
mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya habari wakiwemo taasisi za
habari, Waandishi wa Habari binafsi, watengenezaji wa maudhui mtandaoni
na Maafisa Habari wa Serikali.
Aidha, Mwasalyanda amesema ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na
ushindani wa haki, maandalizi ya tuzo hizo yanahusisha pia Bodi ya
Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia
weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuzingatia
matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Amesema kabla
ya mashindano hayo, mwaka jana TCRA na TAMWA waliendesha mafunzo maalumu
yaliyowanufaisha zaidi ya Waandishi wa Habari 2,000, hatua iliyochangia
ongezeko la maudhui ya ndani yenye ubora na tija kwa jamii.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa TAMWA, Dkt. Kannaeli Kaale, amesisitiza
umuhimu wa Waandishi wa Habari kutumia tuzo hizo kama jukwaa la kuibua
na kusimulia mafanikio ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili
wananchi na dunia kwa ujumla ziweze kutambua hatua zinazopigwa.
“Nasisitiza
waandishi wa habari kushiriki kuwania Tuzo za Habari za Maendeleo za
Samia Kalamu Awards 2026, kwa kuwa waandishi wa habari ndio daraja kati
ya serikali na wananchi, tuendelee kuandika habari za miradi ya
maendeleo, tuone umuhimu wa kusemea miradi yetu hatua tunazopiga za
kimaendeleo. Naomba muachane na maneno kwamba kushiriki tuzo hizi ni
kwamba umenunuliwa, siyo kweli.” amesema Dkt. Kaale.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula,
amewahimiza Waandishi wa Habari wenye ithibati kushiriki kwa wingi
katika mashindano hayo, akisisitiza kuwa mwaka huu ithibati ni miongoni
mwa vigezo vya ushiriki.
“Mtakumbuka Msimu wa kwanza wa Samia Kalamu mambo ya JAB hayakuwepo, kwa hiyo waandishi walishiriki wote bila kujali vigezo vya Ithibati lakini mwaka huu kuna hiki kigezo cha kuwa na ithibati kwa hiyo niwashauri basi wote wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati, wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.” Amesema Wakili Kipangula na kuongeza;
“Ni muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isije ikaonekana ni tuzo za watu fulani tu, kila mmoja awasilishe habari hasa zile ambazo zimezingatia maadili, zimezingatia weledi, lakini pia habari ambazo zina impact kwa kwa wananchi,” amesema Kipangula.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mchakato wa kupokea kazi umeanza rasmi Mei 31 na utafungwa Juni 30, 2026 kupitia tovuti ya samiaawards.tz, huku tuzo hizo zikitarajiwa kutolewa kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu.













No comments:
Post a Comment