Mwenyekiti wa Airtel Africa Foundation Plc, Segun Ogunsanya.
-Vijana na wanawake 30,530 wawezeshwa na mafunzo ya ufundi stadi
Airtel Africa Foundation imechapisha ripoti yake ya kwanza, inayoonyesha utekelezaji wa miradi yenye mchango chanya kwa jamii katika nyanja mbalimbali kama vile upatikanaji wa elimu, kuwajengea watu ujuzi wa kigiditali pamoja na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa mamilioni ya waafrika.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26, Taasisi ya Airtel Africa Foundation ilitenga jumla ya Dola 6.2 milioni kwa ajili ya miradi inayotekelezwa chini ya nguzo zake nne za kimkakati za FEED ambayo ni Ujumuishi wa Kifedha, Elimu, Utunzaji wa Mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo pamoja na Ujumuishi wa Kidijitali. Sambamba na nguzo tajwa elimu ni moja kati ya eneo lilopokea sehemu kubwa zaidi ya uwekezaji.
Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyorekodiwa ni pamoja na kuunganishwa kwa shule 1,028 kwenye huduma za intaneti kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na UNICEF. Hii imeongeza idadi ya shule zilizounganishwa kufikia 3,296 katika nchi 13 za Afrika ikiwemo Tanzania, zikihudumia zaidi ya wanafunzi milioni 2 na walimu karibu 39,000.
Aidha, majukwaa 64 ya kidijitali ya kujifunzia bila malipo yamewezesha zaidi ya wanafunzi milioni 11 kupata maudhui ya elimu bila gharama yoyote, huku yakichochea mafunzo kidijitali katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika.
Katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, Airtel Africa Foundation ilifanikiwa kukamilisha ukarabati mkubwa wa shule saba (7) za umma na kuendelea na maboresho katika shule nyingine 43 kupitia Mpango wa Kuasili Shule (Adopt School).
Mpango huo unalenga kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza upatikanaji wa teknolojia za kidijitali na kukuza maendeleo ya mwanafunzi kwa ujumla.
Kupitia programu ya mafunzo ya kiteknolojia inayofahamika kama Airtel Africa Tech Fellowship, jumla ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu 257 ulitolewa kwa wanafunzi nchini Malawi, Nigeria, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Mpango huo unaendelea kupanua fursa za elimu ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati) huku ukijenga kizazi kipya cha wataalamu wa teknolojia wenye ushindani wa kimataifa.
Vilevile, vijana na wanawake 30,530 walipatiwa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia programu mbalimbali zilizotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi za kitaifa, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta binafsi.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mwenyekiti wa Airtel Africa Foundation, Segun Ogunsanya, alisema:
"Airtel Africa Foundation ilianzishwa kwa lengo la kusaidia kuondoa vikwazo vinavyotokana na ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa fursa. Ingawa bara la Afrika limejaliwa kuwa na vipaji vingi lakini bado wengi hukosa fursa hasa katika upatikanaji wa elimu, ukosefu wa zana za kidigitali na vikwazo vya kiuchumi. Kupitia wigo wetu mpana tumejizatiti kuwekeza kwa jamii ambazo fursa hizi muhimu bado hazijawahikia."
Ripoti hiyo pia inaonesha mwelekeo wa Airtel Africa Foundation katika kuwekeza kwenye miradi yenye matokeo na yenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya muda mrefu katika jamii. Katika mwaka ujao, Airtel Africa Foundation inalenga kupanua zaidi programu zake kwa kuongeza idadi ya shule zinazonufaika kupitia Mpango wa Kuasili Shule (Adopt School) kwa kufikia zaidi ya shule 80, kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana zaidi ya 600, kuunganisha shule nyingine 2,000 kwenye huduma za intaneti bila malipo, pamoja na kupanua programu za ujuzi wa kidijitali na ujumuishi wa kifedha katika jamii ambazo bado hazijafikiwa kikamilifu.
"Kama taasisi, tupo katika nafasi ya kipekee ya kuchochea maendeleo ya ujuzi, kuongeza uwezo wa kiuchumi wa watu binafsi na kaya, na kushirikiana na serikali katika kufungua fursa za mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika kwa kiwango kikubwa zaidi," aliongeza Ogunsanya.
Ripoti Kamili ya Mwaka ya Airtel Africa Foundation 2025/26 inapatikana kupitia tovuti ya Airtel Africa Foundation.


No comments:
Post a Comment