HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 31, 2026

CCM Geita Yafunga Kampeni za Uchaguzi wa Udiwani Kata ya Bwongera kwa Kishindo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimehitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Bwongera, Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Kampeni hizo zilianza rasmi Mei 11, 2026 katika Kijiji cha Bwongera na zimefikia tamati leo katika Kijiji cha Mkolani, Kata ya Bwongera.
Akizungumza wakati wa kufunga kampeni hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, amemtaka mgombea wa chama hicho, Donald Zacharia, kuhakikisha anashughulikia changamoto zinazowakabili wananchi, hususan tatizo la wanyama wakali na waharibifu kama viboko na mamba kutokana na kata hiyo kuwa pembezoni mwa Ziwa Victoria. 
Amesema ni muhimu kwa kiongozi huyo kuyafikisha malalamiko ya wananchi kwenye mamlaka husika ili yatafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wake, mgombea huyo wa CCM, Donald Zacharia, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Ualimu, ameomba ridhaa kwa wananchi kumpigia kura katika uchaguzi unaofanyika kesho. Amesema katika kipindi chote cha kampeni ametembelea vijiji mbalimbali vya kata hiyo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.
Ameahidi kushughulikia changamoto zilizo ndani ya uwezo wake na kuziwasilisha kwa mamlaka zinazohusika zile zinazohitaji maamuzi ya ngazi za juu ili zipatiwe ufumbuzi.
Kata ya Bwongera imekuwa wazi baada ya aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, Batholomeo Manunga, kuvuliwa uanachama wa CCM na hivyo kupoteza sifa za kuendelea kushika nafasi hiyo.
Jumla ya vyama sita vya siasa vinashiriki uchaguzi huo, ambavyo ni United Democratic Party (UDP), ACT Wazalendo, CHAUMMA, Civic United Front pamoja na CCM.
Wananchi wa Kata ya Bwongera wanatarajiwa kupiga kura kesho kuchagua diwani watakayemwona anafaa kuwaongoza kwa kuzingatia sera na ahadi zilizowasilishwa na wagombea wakati wa kampeni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad