HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 21, 2026

AIRTEL YAFUNGUA DUKA LA KIDIJITALI KUIMARISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO NA FEDHA MTANDAONI

 




KAMPUNI ya Airtel Tanzania imezindua Duka la Kidijitali (Smart Shop) katika Mkoa wa Mwanza, hatua inayolenga kusogeza karibu zaidi huduma za mawasiliano, Airtel Money na intaneti kwa wananchi wa Ukanda wa Ziwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mkalipa, aamesema uwekezaji huo unaonesha wazi jinsi teknolojia inavyochochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

“Teknolojia ni daraja la maendeleo, na mawasiliano ni nyenzo muhimu inayowaunganisha watu, biashara na fursa mbalimbali,” amesema Mkalipa.

Ameongeza kuwa Mwanza inaendelea kukua kama kitovu cha biashara katika Ukanda wa Ziwa kutokana na shughuli za uvuvi, kilimo, madini, biashara na usafirishaji zinazotegemea zaidi huduma za mawasiliano.

“Si tu ufunguzi wa duka, bali ni sehemu ya mabadiliko mapana ambapo teknolojia inaleta huduma karibu zaidi na wananchi na kuunda fursa mpya za kiuchumi,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Mwanza una wakazi takribani milioni 3.69, hali inayoonyesha ukubwa wa soko na umuhimu wa huduma za kidijitali.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Airtel Tanzania Kanda ya Ziwa, Mlaki Mchala, amesema Mwanza ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali.

“Mwanza ni miongoni mwa maeneo yetu yanayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali,” amesema Mchala.

Ameeleza kuwa Airtel Tanzania kwa sasa inahudumia zaidi ya wateja milioni 1.2 katika Mkoa wa Mwanza na ina mtandao wa zaidi ya mawakala 15,000 wa Airtel Money.

“Biashara za leo zinategemea sana mawasiliano na malipo ya kidijitali. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanabaki wameunganishwa wakati wote,” ameongeza.

Airtel Tanzania imesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha huduma za mawasiliano na kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.

Duka hilo la kidijitali linatoa huduma za usajili wa laini, Airtel Money, mauzo ya simu janja, huduma za intaneti na msaada wa kidijitali kwa wateja.

Mwanza, maarufu kama “Rock City,” inaendelea kuvutia uwekezaji kutokana na miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa maeneo ya biashara na maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad