SERIKALI imesema uzalishaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku umepungua kwa asilimia 95 hatua iliyochangia kupungua kwa uzalishaji wa taka za plastiki katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa bungeni jijini Dodoma leo Aprili 29, 2026, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Dkt. Catherine Joachim aliyetaka kujua Serikali imepata matokeo gani katika kupunguza uchafuzi wa mazingira tangu kuanza kwa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki mwaka 2019.
Akijibu swali hilo Mhe. Kwagilwa alibainisha kuwa baada ya katazo hilo kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya plastiki kiliongezeka kutoka kutoka chini ya asilimia 40 mwaka 2018 hadi kufikia zaidi ya asilimia 85 mwaka 2026.
Kutokana na hatua hiyo, alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuzingatia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ajili ya kulinda afya na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa taka za plastiki katika maeneo ya fukwe za bahari na maziwa zimepungua kwa takribani asilimia 60 hivyo kupunguza hatari kwa viumbe wa majini.
Halikadhalika, Mhe. Kwagilwa alieleza kuwa katazo la mifuko ya plastiki limesaidia kupungua kwa gharama za kuzibua mitaro ya maji machafu kwa wastani wa asilimia 30 hadi 40, kwani mifuko ya plastiki ilikuwa chanzo kikuu cha uzibaji wa miundombinu hiyo.
Akijibu maswali ya nyongeza, alibainisha kuwa Serikali imeweka jitihada madhubuti za kuhakikisha taka hususani zile za plastiki zinazozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini zinarejelezwa na kuzalisha bidhaa.
Pia, alisema Serikali inahakikisha kwenye majiji kwa mfano Dar es Salaam, inajenga madampo makubwa yatakayoambatana na viwanda vitakavyofanya shughuli ya urejelezaji na kuchakata taka kuwa bidhaa, hatua itakayosaidia kudhibiti taka.
Ifahamike kuwa mifuko ya plastiki ni aina ya mifuko yenye mchanganyiko wa kemikali zisizooza hivyo kuleta athari kwenye mazingira pamoja na afya kwa binadamu na wanyama.
Aidha, kutokana na tafiti mbalimbali mifuko ya plastiki huchukua miaka 400 hadi 1000 kuoza ardhini na hivyo kuleta athari mbalimbali zikiwemo kuathiri mifumo ikolojia ya bahari ambapo inakadiriwa 100,000 viumbe bahari na ndege bahari millioni moja kila mwaka wanakufa kwa kula mifuko ya plastiki.
Athari zingine ni pamoja na kuchafua miji kutokana na kushindwa kuoza, kuathiri mifugo kutokana na kula mifuko ya plastiki, kuharibu miundombinu kwa kuziba kwenye mifereji na baadhi ya njia za maji, kubeba na kusambaza viumbe vamizi na bakteria na pia inapochomwa moshi wake una madhara na unaweza kusababisha maradhi ya kansa.

.jpg)
No comments:
Post a Comment