WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amezindua makati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili wa mwaka 2026/27 hadi 2036/37, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mustakabali wa Taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makonda amesema mkakati huo unatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Septemba 24, 2024 mkoani Ruvuma wakati wa Tamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni, ambapo alielekeza kuandaliwa mfumo wa pamoja wa kitaifa utakaounganisha nguvu za Serikali, familia na wadau wote kulinda utambulisho wa Watanzania.
Amesema maadili ni msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yoyote, yakitoa mwelekeo wa fikra, mienendo na maamuzi ya jamii katika nyanja zote, huku akibainisha kuwa Katiba ya mwaka 1977 kupitia Ibara ya 9 inaweka misingi ya Utu, Umoja, Usawa, Utaifa na Uwajibikaji kama nguzo za maisha ya Mtanzania.
Makonda amesema licha ya fursa zinazotokana na maendeleo ya sayansi, teknolojia na utandawazi, bado kuna changamoto ya mmomonyoko wa maadili ikiwemo kupungua kwa uwajibikaji, kudhoofika kwa taasisi ya familia, matumizi yasiyofaa ya mitandao, kuongezeka kwa uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeandaa mkakati wa miaka 10 unaolenga kujenga jamii yenye maadili imara inayozingatia utu, uwajibikaji, uzalendo na mshikamano wa kitaifa". Amesema Makonda
Amesema kuwa mkakati huo umezingatia maeneo muhimu ikiwemo kuimarisha taasisi ya familia, kuboresha urithishaji wa maadili kupitia elimu, kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia na mitandao, pamoja na kuimarisha usimamizi wa sheria na kanuni zinazolinda maadili ya jamii.
Amesema mkakati huo umeandaliwa kwa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi, taasisi za dini, wasanii, vijana na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha unakuwa na uhalisia na umiliki wa pamoja.
Aidha, Makonda ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza maadili, akisisitiza kuwa zaidi ya asilimia 42 ya Watanzania ni watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 15, hivyo kuna wajibu wa pamoja kujenga msingi imara wa kimaadili kwa kundi hilo.
Amewataka wazazi na walezi kuwajibika katika malezi, viongozi wa dini na jamii kuhamasisha maadili, wasanii na wazalishaji wa maudhui kuzalisha kazi zinazojenga jamii, vyombo vya habari kuelimisha umma, na mamlaka za udhibiti kuimarisha utekelezaji wa sheria.
"Utekelezaji wa mkakati huu utaanzia ngazi ya familia hadi Taifa, Serikali inaahidi kuhakikisha wadau wote wanapata elimu na taarifa za mkakati huo kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kwani bila maadili imara, maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa.

.jpeg)


No comments:
Post a Comment