Fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati zimefunguliwa kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Maelewano (MoU) kati ya Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) na National Export Promotion Council of Belarus.
Hafla ya utiaji saini ilishuhudiwa na Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji.

Makubaliano hayo yanafungua milango ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi, zikiwemo kilimo, viwanda na usindikaji, biashara ya bidhaa na huduma, teknolojia, madini, nishati, vifaa tiba, usafirishaji pamoja na upanuzi wa masoko ya kimataifa kwa bidhaa za Tanzania na Belarus.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mahmoud Thabit Kombo alisema ushirikiano huo unaweka msingi imara wa kupanua mahusiano ya kiuchumi yenye manufaa kwa mataifa yote mawili na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Maxim Ryzhenkov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, alisema nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano wa vitendo utakaozalisha matokeo chanya ya kiuchumi na kibiashara kwa pande zote mbili.
Akizungumzia umuhimu wa makubaliano hayo kwa sekta binafsi, Rais wa Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC), Vicent Minja alisema MoU hiyo ni daraja muhimu la kufungua biashara na uwekezaji zaidi, akisisitiza utekelezaji madhubuti wa makubaliano hayo ili kuleta matokeo halisi.
Kupitia makubaliano hayo, Tanzania na Belarus zinatarajiwa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza ubadilishanaji wa teknolojia na maarifa, kuchochea miradi ya pamoja pamoja na kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia masoko mapya na fursa za kimataifa.







No comments:
Post a Comment