▫️Hatua kubwa kwa maendeleo ya Ngumi Kimataifa
20-03-2026 - Dar es Salaam.
SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT) linapenda kuutaarifu umma na wadau wa mchezo wa ngumi kuwa Tanzania imekuwa rasmi mwanachama wa World Boxing, Shirikisho la Kimataifa la Ngumi linalotambuliwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC).
Uamuzi wa kuipokea Tanzania ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya World Boxing kilichofanyika tarehe 15-03-2026, ambapo Tanzania iliungana na mataifa mengine nane yaliyopitishwa kuwa wanachama wapya.
Mataifa hayo ni Zambia, Msumbiji, Urusi, Tonga, Cyprus, Belarus, Niue na Papua New Guinea.
Kwa uamuzi huo, World Boxing sasa ina jumla ya wanachama 168 duniani, hatua inayoendelea kuimarisha ukuaji na usimamizi wa mchezo wa ngumi kimataifa.
World Boxing imepewa dhamana na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kusimamia na kuratibu mashindano ya ngumi katika matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo Michezo ya Olimpiki, Michezo ya Jumuiya ya Madola, pamoja na Michezo ya Kimabara kama African Games.
Akizungumzia mafanikio hayo, Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Ndg. Lukelo Willilo, amesema:
“Kupatikana kwa uanachama wa World Boxing ni hatua muhimu na ya kihistoria kwa maendeleo ya ngumi nchini Tanzania. Fursa hii itawawezesha mabondia wetu kushiriki kikamilifu katika mashindano ya kimataifa na kuongeza ushindani pamoja na viwango vyao. Tunaendelea kujipanga kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na uanachama huu.”
Kupatikana kwa uanachama huu ni hatua muhimu kwa maendeleo ya mchezo wa ngumi nchini Tanzania, kwani utafungua fursa zaidi kwa mabondia kushiriki mashindano ya kimataifa na kukuza viwango vya ushindani.

No comments:
Post a Comment