Na Mwandishi Wetu
SERIKALI inaendelea kujipanga kutunga sheria jumuishi zitakazoshirikisha sekta binafsi kwa lengo la kuimarisha uwezo wa wanawake katika uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora na ushindani katika soko la kimataifa.
Akizungumza Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema hatua hiyo inalenga kuwapa wanawake mazingira bora ya uzalishaji na biashara ili waweze kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi jumuishi unaowashirikisha wanawake na vijana kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kapinga alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutenga asilimia 30 ya zabuni za manunuzi ya umma kwa makundi maalum, yakiwemo wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum, hatua inayosaidia kukuza biashara na kuongeza kipato kwa makundi hayo.
Alitoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) pamoja na msimu wa sita wa utoaji wa tuzo za Viwanda na Biashara kwa wanawake wajasiriamali yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kuwaongezea wanawake uwezo wa kupata elimu ya teknolojia bunifu ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na kukidhi viwango vya soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Rais wa TWCC, Mercy Sila, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuboresha mazingira ya biashara nchini, akisema maboresho katika upatikanaji wa mitaji kupitia madirisha ya wanawake katika benki na mifuko ya uwezeshaji yamepunguza changamoto za upatikanaji wa fedha kwa wanawake wafanyabiashara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema chemba hiyo inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali ili kuwawezesha wanawake kupata mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji na masoko ya kimataifa.
Alisema kupitia juhudi hizo, wanawake wengi wameanza kupanua biashara zao na kupata fursa ya kupeleka bidhaa zao katika masoko ya nje ya nchi, jambo linalochangia kukuza uchumi wa taifa.



.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment