Na WMJJWM- Uturuki
TANZANIA na Uturuki zimekubaliana kuanzisha makubaliano yatakayowezesha vijana kutoka Tanzania kunufaika na fursa za mafunzo, uzoefu wa biashara na kuunganishwa na vijana wenzao kupitia Jukwaa la Young MÜSIAD ili kukuza mtandao wa biashara, ujuzi na kutengenenza rasilimaliwatu itakayoimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati wa ziara ya kikazi nchini Uturuki tarehe 18 Desemba 2025.
Kupitia mazungumzo hayo, Viongozi hao walijadili fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki kwenye maeneo ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia programu za uanagenzi, ubunifu, teknolojia na ziara za mafunzo (exchange programs) ili kuwezesha vijana kunufaika na utaalamu kwenye sekta ya biashara.
Dkt. John amesema hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba Tanzania na Uturuki ni washirika wazuri kwenye sekta ya biashara na nchi hizo mbili zina dhamira ya kukuza ushirikiano huo ili kuchochea ongezeko la urari wa biashara na manufaa ya kiuchumi yatokanayo na sekta hiyo.
Dkt. Jingu amesema katika kufanyia kazi masuala muhimu yaliyokubalika kwenye kikao hicho, Tanzania itaandaa na kuwasilisha rasimu ya hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano huo pamoja na maeneo mengine ambayo nchi inaweza kunufaika kupitia Jumuiya ya MÜSIAD, hususan uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia sekta za ujasiriamali na biashara
"Jumuiya ya MÜSİAD ni mahiri nchini Uturuki na duniani ina uzoefu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya biashara na uchumi, ikiwa na wanachama zaidi ya 60,000 kwenye sekta 25 hivyo katika makubaliano haya tutafaidika sana katika kuhakikisha vijana na Wanawake wa Kitanzania wanapata fursa hizo" amesema Dkt. Jingu
Ameongeza kuwa kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopo, Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuimarisha ushirikishwaji wa vijana kiuchumi ikilenga kuwapa ujuzi (soft skills) lengo likiwa ni kuendesha shughuli zao kwa weledi na kuinua uchumi wao.
Aidha Dkt. Jingu akiwa kwenye ziara hiyo alikutana na kuzungumza na Uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda (MÜSİAD) na Shirika la Women and Democracy Foundation (KADEM) za nchini Uturuki.
Pia Dkt. Jingu alifanya mazungumzo na Bw. Osman Nuri Önügören, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Diplomasia mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa na Watendaji mbalimbali wa jumuiya hiyo.


.jpeg)

No comments:
Post a Comment