Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amelitaka Shirika la Kuhudumia Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kuendelea kuongeza kasi ya kupanga na kuratibu maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Katambi ametoa wito huo leo, Desemba 19, 2025, jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za SIDO na kuzungumza na watumishi wa shirika hilo.
Amesema uzoefu wa nchi nyingi zilizoendelea unaonesha kuwa maendeleo yao ya kiuchumi yalianzia katika kukuza viwanda vidogo, ambavyo baadaye vilikuzwa na kuwa viwanda vya kati na vikubwa, hatua iliyoongeza ajira na pato la Taifa.
Naibu Waziri huyo amewasisitiza watumishi wa SIDO kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha shirika hilo linaanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Pia amewataka watumishi wanaopata fursa ya kwenda nje ya nchi kwa kazi kuhakikisha safari hizo zina mlengo wa kujifunza na kupata uzoefu kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Mimi na Mheshimiwa Waziri Kapinga tumekuja kuunga mkono na kuendeleza mambo mazuri yanayofanyika katika Wizara hii. Tunategemea kuona mabadiliko chanya kwa kuhakikisha vijana wajasiriamali wanajiajiri kupitia viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa,” amesema Katambi.
Ameongeza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ipo tayari kusikiliza mawazo bunifu kutoka kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuzalisha ajira zaidi, hususan kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Serikali imedhamiria, kupitia sera zilizoboreshwa, kuhakikisha kunazalishwa ajira za kutosha na zenye tija ili kuwanufaisha vijana wetu na Watanzania kwa ujumla,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Silvester Mpanduji, amesema shirika hilo limejipanga ndani ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni moja kwa wajasiriamali nchini.
Aidha, Mpanduji ameongeza kuwa SIDO tayari imeanza uwekezaji kwa njia ya ubia katika mikoa minane nchini, hatua inayolenga kukuza viwanda vidogo na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Friday, December 19, 2025
Home
Unlabelled
SIDO Yapongezwa, Katambi Aagiza Kuongeza Kasi
SIDO Yapongezwa, Katambi Aagiza Kuongeza Kasi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)















No comments:
Post a Comment