HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 20, 2025

MMOJA ATUHUMIWA KUISABABISHIA TRA HASARA YA SH MILIONI 950

 


MFANYABIASHARA Frank Kalage anayetuhumiwa kwa makosa manne likiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh Milioni 954.5 ameiomba kuwepo na ukomo wa kupatikana kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) cha kuruhu kesi hiyo kusikilizwa Mahakama ya Kinondoni.

Washtakiwa wengine ni Awadhi Mhavile, Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga mafundi wa mashine za EFD na Salma Ndauka (38) Msimamizi wa Gereji, wote kwa pamoja na Kalage wanatuhumiwa kwa makosa saba.

Mfanyabiashara huyo, alifikia uamuzi huo jana wa kutoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Is-hqa Kuppa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Serikali Auni Chilamula akisaidiana na Sada Mohamed, aliieleza Mahakama kuwa kesi iliitwa kutajwa, bado wanasubiri kibali 'Consent' kutoka kwa DPP ili waweze kuendelea na pia wanaomba kuahirishwa hadi watakapopata kibali hicho.

Baada ya kudai hayo, Hakimu Kuppa alisema kama kuna mtu yeyote anataka kuzungumza anyooshe kidole, ndipo Kalage akanyoosha na hakimu alimpa nafasi ya kuzungumza.

"Mheshimiwa nakumbuka kikao cha mwisho cha mahakama (session) Wakili John Mwakifuna alidai consent haijasainiwa na sasa wanasema vilevile, tu naomba kuwe na ukomo wa jambo hili,"alidai Kalage

Hakimu Kuppa, alimueleza Auni kwamba yanayosemwa wawe wanaandika na kupeleka kwa wakili mwenzako sababu suala hilo alishaliongelea kikao kilichopita.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 4, 2025.

Ilidaiwa kuwa kati ya Mei 17 na Julai 2023, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walitumia isivyohalali mashine za EFD zilizozuiwa kinyume na sheria kutengeneza risiti zisizo halali zilizopakiwa kwenye mfumo wa TRA na kuwezesha walipa kodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 954,596,372 na kumpotosha Kamishina wa mamlaka hiyo.

Pia washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutumia isivyo halali mashine za EFD zilizokuwa zimefungiwa na kumdanganya Kamishna wa TRA kwa kutoa risiti zisizosahihi hivyo, kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372.

Aidha katika mashtaka la tatu yanayomkabili Mhavile peke yake inadaiwa, Julai 8 mwaka 2023, mshatakiwa huyo alikutwa na mashine za kielektroniki 22 zinazozaniwa kuwa za wizi au zimepatikana kwa njia isiyo halali.

Wakili alidai kudai kuwa, Julai 19, mwaka jana maeneo ya Sinza A, Wilaya ya Kinondoni, Ndauka alikutwa na mashine 10 za EFD zidhaniwazo kuwa za wizi au kuchukuliwa kwa njia ya isivyohalali.

Katika mashataka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Mei 13 na Julai mwaka 2023, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa kutumia mashine hiyo walitoa risiti zisizohalali zilizotumiwa na walipakodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 954.5 kwa TRA wakati wakijua kwamba fedha hizo ni zao la kosa la kuisababishia serikali hasara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad