Mchungaji wa Kanisa KKKT Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Emmanuel Luoga,akizungumza kwenye mdahalo maalum wa kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru uliofanyika leo kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari Nasuli wilaya Namtumbo ambapo amewataka vijana humo kuhakikisha wanafanya kazi ili kujiletea maendeleo yao.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma,wakifuatilia mdahalo wa sherehe za miaka 63 ya Uhuru uliofanyika katika shule ya Sekondari Nasuli wilaya humo.
Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Salum Ali Salum(hayupo pichani)wakati wa mdahalo maalum wa kusherehekea miaka 63 ya Uhuru uliofanyika katika Bwalo la shule ya Sekondari Nasuli wilayani humo.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,Salum Ali Salum akipanda mti wa mbao kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Nasuli wilaya Namtumbo baada ya kumalizika kwa mdahalo maalum wa sherehe ya miaka 63 ya Uhuru mdahalo uliofanyika katika shule ya Sekondari Nasuli wilayani humo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma Ambokile Paul,akipanda mti kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Nasuli wilayani Namtumbo mara baada ya mdahalo maalum wa sherehe za miaka 63 za Uhuru wa nchi yetu.
Na Muhidin Amri, Namtumbo
WATANZANIA wametakiwa kudumisha amani,umoja,upendo na mshikamano wa kitaifa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho ili kuendeleza misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa letu Hayati Julius Nyerere na Abeid Mani Karume.
Wameaswa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoashiria vurugu na uvunjifu wa amani wakati huu tunasherehekea miaka 63 tangu ilipopata Uhuru wake mwaka 1961.
Hayo yamesemwa leo kwenye mdahalo wa miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Nasuli Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Chifu Shaphi Mwenyengoma ameipongeza Serikali kwa kutambua na kutoa fedha nyingi ambazo zimesaidia kukamilisha miradi mbalimbali iliyopo kwenye maeneo yao ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya,Hospitali na huduma ya maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Chifu Mwenyegoma ni kwamba,tangu nchi yetu ipate Uhuru kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo,ujenzi wa shule za msingi na Sekondari na kuimarika kwa huduma ya usafiri na usafirisha na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kusafirisha mazao yao kutoka shambani kupeleka sokoni.
Chifu Mwenyegoma alitaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 63 ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya barabara ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha wananchi wa Namtumbo kujikomboa na umaskini.
Mchungaji wa kanisa la KKKT Namtumbo Emmanuel Luoga,amewaasa vijana kutumia miaka 63 ya Uhuru kufanya kazi za kujiletea maendeleo badala ya kutumia muda wao mwingi kukaa vijiweni na kucheza bao hali inayopelekea kukithiri kwa kiwango cha umaskini miongoni mwa vijana wengi wa wilaya hiyo.
Alisema,kwa upande wa Serikali tayari imetimiza wajibu wake kwa kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya, hivyo kazi iliyobaki ni kwa vijana wenyewe kuchangamkia uwekezaji uliofanywa na Serikali yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
“licha ya Serikali kufanya kazi kubwa kutuletea maendeleo katika nyanja mbalimbali,lakini bado kundi la vijana linaendelea kuwa mzigo kwa kushindwa kufanya kazi za kujipatia kipato na wengine kuendelea kuwa tegemezi kwa wazazi wao jamboa amblo siyo sahihi wakati huu ambao tumefikisha miaka 63 tangu tupate Uhuru”alisema.
Ametoa wito kwa vijana, kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vyote vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani hapa nchini kwa kuweka uzalendo mbele na kujali maslahi mapana ya Taifa letu.
Katibu wa Chama cha Wananchi(CUF) wilaya ya Namtumbo Rashid Mfaume,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada kubwa inayofanya ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Alisema,Chama hicho kitaendelea kuunga mkono Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo yenye lengo la kuinua maisha ya wananchi ili kuharakisha kukua kwa uchumi wa nchi yetu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya alisema,kwa muda wa miaka 63 wilaya ya Namtumbo imepiga hatua kubwa katika nyanja za mawasiliano,usafirishaji na uboreshwaji wa sekta ya kilimo.
Malenya alitolea mfano Halmashauri ya wilaya Namtumbo wakulima wake wameendelea kunufaika na mapato yatokanayo na kilimo kwa mazao mbalimbali yanayolimwa katika wilaya hiyo kutokana na upatikanaji wa mbolea za ruzuku na bei nzuri ya mazao yao.
Malenya ambaye aliwakilishwa na Afisa Tarafa wa Mkongo Salum Ali Salum alisema,hali hiyo inatokana na misingi mizuri iliyowekwa na Baba wa Taifa na kutekelezwa na viongozi wa awamu zote tano na sasa misingi hiyo inaendelezwa na Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan.
Malenya alisema,maadhimisho ya Uhuru wetu hayana budi kuturejesha kipindi cha nyuma yaani kabla ya Uhuru na sasa ili kutukumbusha umuhimu wa Uhuru wetu na maendeleo yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuimarika kwa amani,umoja na mshikamano jambo ambalo ndiyo msingi wa maendeleo yetu.
No comments:
Post a Comment