HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 2, 2024

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo-wajibu kwa Wananchi wa Zanzibar kuonyesha mshikamano katika kupigania haki zao za msingi


Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Taifa, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni wajibu kwa Wananchi wa Zanzibar kuonyesha mshikamano katika kupigania haki zao za msingi, zikiwemo za Utambulisho, pamoja na Maslahi ya Nchi yao.

Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Jumatatu Disemba 02 2024, akijibu hoja mbali mbali kutoka kwa Wananchi wa Kijiji cha Muwi, Shehia ya Mjananza Wingwi, Jimbo la Pandani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hiyo ilikuwa ni Hafla Maalum ambayo Mheshimiwa Othman alipojumuika na Wananchi hao, ambao pia wameitumia fursa hiyo, kueleza changamoto na kero mbali mbali zinazowakabili.

Amesema wajibu huo unakuja kutokana na baadhi ya Viongozi wa Serikali wasiofuata Maadili, Miongozo na Misingi ya Uongozi, bali huendekeza 'vilemba vya kisiasa', kwa kuwagawa Wananchi na hata kukandamiza haki zao.

Akifafanua kauli hiyo Mheshimiwa Othman amesema yapo mambo mengi ya msingi pia yameainishwa katika Katiba ya Zanzibar, bali wapo Viongozi ambao wanayapindisha kwa kuendekeza maslahi yao binafsi.

Hivyo amesema, hapana- budi kuungana pamoja kwa kuyakataa hayo, na kisha kuiweka madarakani ACT- Wazalendo, kwaajili ya kuja kulinda Heshima, Utu, Thamani ya kila Mtu, pamoja na Katiba ya Zanzibar.

"Katiba ya Zanzibar imebainisha wazi wazi kwamba ili uwe Mgombea wa Urais, ni lazima uwe ni Mzanzibari wa Kuzaliwa; sasa kama Serikali hiyo hiyo haitoi Vyeti vya Kuzaliwa kwa Wananchi Wazawa na Wenye haki, maana yake ni kuandaa mazingira Nchi kutawaliwa na Wageni na pia Watu

Wasiokuwa na Uchungu nayo", amesisitiza Mheshimiwa Othman huku akiwataka Wananchi kukiwajibisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwaondoa madarakani kupitia Sanduku la Kura, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa hapo Mwakani.

Mheshimiwa Othman ameongeza kwa kusema, "Mwenendo wa baadhi ya Viongozi, hasa wa Ngazi ya Sheha, Wilaya na Mikoa, ambao Kisheria ni Watumishi wa Umma, kujivisha zaidi Wajibu, Itikadi na Chuki za Vyama vyao vya Siasa, na ikibidi hata kuwanyima haki Wananchi wengine, ni kuukosea Umma, hivyo yapasa kuwang'oa madarakani, na kutafuta mbadala, ili pia kurudisha nidhamu katika Kuongoza Nchi".

Msisitizo huo wa Mheshimiwa Othman umekuja, kufuatia hatua ya Sheha wa Shehia ya Mjanaza Wingwi, Bw. Hamad Said Ali, kuibuka mbele ya Hadhara hiyo, na kudai kuwa yeye ni Kada, Mkereketwa, na Mfuasi anayeitumikia CCM katika kutekeleza Majukumu yake, huku akisahau kwamba ni Mtumishi na Muwakilishi wa Serikali, kwa Ngazi ya Jamii; licha ya Wananchi waliokuwepo hapo, akiwemo Bi. Zuwena Omar Makame, kumyooshea kidole Kiongozi huyo kutokana na khulka yake ya Ubaguzi, na Ukandamizaji wa haki, mwenendo ambao wamesema ni kikwazo dhidi ya juhudi zao za kujiletea maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Ndugu Omar Ali Shehe, amesema kilichobakia kwa CCM na Sehemu kubwa ya Waliowapa Mamlaka, wakiwemo Idadi kubwa ya Viongozi wa Shehia, ni hila ni ufuasi wa mbinu chafu kwa wananchi, hasa wale wasiowaunga mkono.

Aidha amesisitiza haja ya Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Awamu ya Mwisho ya Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, hapo mapema Mwezi wa Februari Mwakani, kama hatua muhimu ya Kupigania Heshima na Mageuzi ya Kweli, ya Kuiongoza Nchi hii.

Akitoa salamu zake, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo wa Mkoa wa Kichama wa Wete, Ndugu Juma Khamis Ali, amesema mwelekeo wao kwa sasa ni kuhamasisha uungwaji mkono mkubwa wa wananchi ili kuja kupata Viongozi Bora, wenye Nidhamu na Maadili, kuanzia wa Ngazi ya Shehia hadi Urais, ili kujenga nidhamu ya Utumishi, kwaajili ya Maslahi ya Umma.

Mara baada ya kusikiliza Kero za Wananchi Mheshimiwa Othman, amekuwa na Mazungumzo Maalum, na Viongozi wa Kamati za Uongozi za Matawi ya Muwi, Mtakawa, Mjananza, Kibendera na Kichangani, pamoja na Wazee Mashuhuri, wa Jimbo la Pandani, wakiongozwa na Kaimu Mratib wa ACT-Wazalendo Kisiwani Pemba, Ndugu Rashid Ali Abdallah.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad