Na – Nihifadh Abdulla
KATIKA siasa za Zanzibar, kampeni zimekuwa uwanja wenye changamoto kubwa kwa wanawake wanaotafuta nafasi za uongozi. Mbali na changamoto za kawaida za kisiasa, wanawake hukabiliana na tatizo kubwa la matamshi ya chuki, udhalilishaji, na matusi ya kijinsia yanayolenga kudhoofisha heshima na utu wao. Hali hii siyo tu inakiuka haki za msingi za wanawake bali pia inakwamisha juhudi za kujenga demokrasia jumuishi.
Malengo ya Maendeleo Endelevu ni ajenda ya kimataifa iliyopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015 kwa ajili ya kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2030. Malengo haya yanahusu changamoto kuu za dunia kama vile umasikini, njaa, afya, elimu, usawa, mazingira, na uchumi. Kuna malengo 17 yenye jumla ya vipengele 169 na vigezo vya kupima mafanikio.
Lengo la tano linazungumzia zaidi suala la usawa wa kijinsia Kufanikisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana katika nyanja zote za maisha.
Matamshi ya chuki dhidi ya wanawake katika kampeni za kisiasa yanajikita kwenye dhana potofu za kijinsia zinashusha utu wa wanawake badala ya hoja zao za kisiasa ambazo zinahitajika kwenye majukwaa.
Zuhura Mussa Karata kutoka Chama Cha Kijamii -CCK amesema kuwa matusi au dhihaka zinatolewa kwenye kampeni zinawavunja moyo na hata kupata woga.”Tunaona wagombea wanaume wanatumia matusi na kejeli kwenye kampeni suala ambalo si sahihi na wakati mwengine unapata woga kunadi sera zako” Amesema Zuhura.
Ameitaka Tume ya Uchaguzi kuangalia suala la udhalilishaji wakati wa kampeni ili kuweka usalama wa wagombea wanawake wakato huo “Wafuasi wao pia wanashangiria kuona unaambiwa huna mume hio sio sahihi” Amemaliza
Wanawake wagombea mara nyingi hutolewa maneno makali kama vile "hawana maadili," "hawafai kuwa viongozi," hajaolewa au hata kushushwa thamani." Misemo ya aina hii inasambazwa kupitia mikutano ya hadhara, wakati wa kampeni za ndani na nje ya vyama.
Raifa Juma Khamis ni mwanachama wa Chama cha Alliance for Democratic Change –ADC ambaye amekuwa kwenye siasa kwa zaidi ya miaka 15 amesema suala la matusi ya nguoni wakati wa kampeni ni jambo linaendelea kuzoeleka kwa nguvu kubwa “Kwanza wagombea washazoea na wengine kabla ya hapo hutafuta taarifa zako mapema ili wakutukane” Amesema.
Raifa anaona hali inawaogopesha wanawake kupambana kuingia kwenye majimbo na kuacha siasa ni kutokana na kudhalilishwa . “Wakati mwengine ndugu wanasema unakwenda kututukanisha huko maana wanajua kitakachoendelea ukingia kwenye siasa” Raifa amesema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, aliwahi kuzungumza juu matamshi ya chuki kama msingi wa kuzingatia haki za binaadam.
Alisema “Matamshi ya chuki ni shambulizi dhidi ya maadili ya uvumilivu, ujumuishi, na heshima kwa haki za binadamu ambazo ni msingi wa jamii zetu. Lazima tuipige vita.”
Chama cha Ukombozi wa Umma –CHAUMMA ni miongoni vya vyama 19 ambavyo kampeni zake zinakuwa zinasuasua kutokana na kukosa rasilimali fedha Fatma Yusuph Mohd ambaye ni mwanachama wa CHAUMMA amesema wakati mwengine wanashindwa hadi kufanya kampeni “Pesa hatuna sasa hio pia inakuwa tatizo maana mshindani wako anapata la kusema”.
Fatma amesema pia kadhia ya kutokuolewa au hata kukaa kwenu inaleta maana mbaya kwa upande wa wanawake waoingia kwenye siasa.” Mwaka 2020 kampeni zilikuwa za nguoni unaona hata aibu kusikiliza” Amesema Fatma.
Maneno ya kashfa kama “hawafai kuwa wake” au “wanapoteza muda wao badala ya kulea familia” yanatolewa ili kuwakatisha tamaa na kudhoofisha imani yao katika uwezo wa kisiasa. Hali hii inalenga kudumisha dhana kwamba wanawake ni wasaidizi wa wanaume na sio viongozi.
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar -TAMWA -Z ni Taasis inayojikita katika kuwasaidia wanawake kwa kuwajengea uwezo na kuwapatia elimu ya udhubutu kwenye masuala ya uongozi na siasa.
Dkt Mzuri Issa ni Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA-Z amesema kuwa vyama vya siasa viwasaidie wanawake kupata ujasiri na kuwakumbusha wanaume kuwa matusi na kuwadhalilisha wanawake kwenye majukwaa ya kisiasa ni uvunjifu wa faragha.” Tume ya Uchaguzi na ZAECA kuona suala hili na kulichukulia hatua zaidi za kisheria” Amesema Dkt Mzuri.
Dkt Mzuri ameshauri “Matusi hayo ni udhalilishaji na kuvunja haki za binadaam na si suala jema hivyo tulikee kwa nguvu zite na Serikali ichukue hatua”.
Matusi yanayotolewa dhidi ya wanawake wagombea mara nyingi hulenga maisha yao binafsi, hali zao za ndoa, au hata mwonekano wao. Badala ya kujadili sera au uwezo wao kuwa viongozi, wapinzani wao hujikita katika kushambulia sifa binafsi.
Mwanaharati wa masuala ya jinsia na haki za Binaadam Almas Ali amesema siasa na masuala binafsi zi vitu vinavyoingilia hivyo wagombea wanawake na wanaume wajitahadharishe na kampeni za matusi kwani ni uvunjivu wa haki za faragha. “Ni Maisha ya kisiasa ya kuona kuna mazoea ya kutukana kwenye kampeni ,ila sasa aina hii ya kampeni ni hatari kwa sababu inawadhalilisha wengine” .
Almas ametoa rai kwa kusema kuwa “Serikali iwachukulie hatua wale wanaopanda kwenye majukwaa ya kampeni na kuanza kuwakashifu wengine. “ Amemaliza.
No comments:
Post a Comment