NA MWANDISHI WETU
MSIMU
wa Nne wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde ulioendeshwa na Benki ya NMB
‘NMB Bonge la Mpango – Mchongo Nd’o Huu,’ umefikia tamati Alhamisi ya
Desemba 19, ambako Dennis Theornest Rwegasira wa Kariakoo Dar es Salaam,
aliibuka mshindi wa jumla wa kitita cha Sh. Mil. 100.
Bonge
la Mpango ilizinduliwa Septemba 25, 2024 na Katibu Tawala Mkoa wa Dar
es Salaam, Dk. Toba Nguvila na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara
wa NMB, Filbert Mponzi, ambapo kwa wiki 12, zilichezeshwa droo za kila
wiki, kila mwezi na fainali kusaka washindi wa pesa na bidhaa zenye
thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 150.
Droo
ya fainali imeendeshwa kupitia Kipindi cha XXL cha Clouds FM,
ikiendeshwa na Mponzi, mbele ya Mkuu wa Mauzo na Mtandao wa Matawi ya
NMB, Doantus Richard na wakuu wengine wa idara mbalimbali za Benki ya
NMB, wakisimamiwa na Afisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania,
Lucy Katamba.
Katika
droo hiyo, Rwegasira ambaye kitaaluma ni Daktari, alipigiwa simu na
kupokea akiwa safarini, ambako licha ya kutoamini ushindi wake, alikiri
kuwa yeye ni mteja mtiifu, mwaminifu na wa muda mrefu, huku akiwataka
Watanzania kuitumia benki hiyo katika huduma zao, akiitaja kama benki
yenye manufaa mengi.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo, Mponzi alisema Bonge la Mpango ni njia moja wapo
inayotumiwa na Benki ya NMB katika kurejesha sehemu ya faida yake kwa
jamii, ndio maana wakabuni wazo la kuja na kampeni hiyo inayolenga
kuhamasisha Watanzania kudumisha utamaduni chanya wa kufungua akaunti na
uwekaji akiba.
“Tunapofunga
kampeni hii, sio mwisho wa kampeni zenye manufaa kwa Watanzania, ipo
NMB MastaBata inaendelea, lakini pia mwaka mpya utaambatana na huduma
nyingi muhimu na nzuri kwa wateja wetu ndio maana tunawawasisitiza kila
mmoja kuhakikisha anafungua akaunti NMB.
“Wakati
tukiwahakikishia wateja wa NMB muendelezo bora wa huduma bora na rafiki
kwao, sisi tunaamini kwamba kila Mtanzania anapaswa kuwa na akaunti
NMB, Benki Bora kwa miaka 11 mfululizo katika miaka 12 iliyopita,”
alisema Mponzi huku akiinadi Akaunti ya Wekeza yenye riba hadi asilimia
12 kwa mwaka.
Ukiondoa
Sh. Mil. 100, katika fainali hiyo walitafutwa washindi saba wa pikipiki
ya mizigo ya matairi matatu (moja kwa kila mmoja), mshindi mmoja wa
trekta ya kilimo ‘power tiller,’ huku washindi wengine wanne kila mmoja
akijinyakulia kitita cha Sh. Mil. 5.
Kupitia
kampeni hiyo, washindi 10 wa kila wiki walijishindia fedha taslimu Sh.
100,000 kila mmoja, huku washindi wengine tisa wakijinyakulia kimoja
kati ya Friji, Televisheni ya kisasa, mashine ya kufulia na jiko la
gesi, kulingana na matakwa ya mteja.
Katika
zawadi za droo za kila mwezi, benki hiyo ilikuwa ikiwazawadia washindi
wanne wa kila mwisho wa mwezi Sh. Mil. 5 kila mmoja, ikiwa na maana
wateja wanane katika miezi miwili ya ya NMB Bonge la Mpango,
waliojizolea Sh. Mil. 40 kwa wote (wakiwemo wanne waliopatikana kwenye
fainali).
NMB
Bonge la Mpango ilianza mwaka 2021, kabla ya mwaka uliofuata (2022)
kurejea tena kwa kampeni hiyo ikitumia kaulimbiu ya ‘2merudi Tena,’
kisha mwaka jana 2023 kuitwa NMB Bonge la Mpango ‘Moto Ule Ule’ na mwaka
huu kuwa NMB Bonge la Mpango ‘Mchongo Nd’o Huu.’
Afisa
Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi
(kulia), akibonyeza kitufe cha kompyuta kuchezesha droo ya kumtafuta
mshindi wa kitita cha Sh. Mil. 100 wa fainali ya Kampeni ya NMB Bonge la
Mpango iliyofanyika katika Studio za Clouds FM jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Afisa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT),
Lucy Katamba na katikati ni mtangazaji wa Kipindi cha XXL cha Clouds FM,
Meena Ally. (Na Mpiga Picha Wetu).
No comments:
Post a Comment