Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amezindua rasmi Bodi ya Shirika la Posta Tanzania huku akilitaka Shirika hilo kuendana na kasi ya Maendeleo ya TEHAMA.
Hafla ya uzinduzi huo imefanyika 18 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa Bodi, Posta House, Jilini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akiwemo Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu, Nicholas Merinyo Mkapa, Naibu Katibu Mkuu, na Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano.
Wengine waliohudhuria ni viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliohudhuria ni pamoja na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Salim Milanzi, Mwenyekiti wa Bodi, Toyi
Ruvumbangu, Makamu mwenyekiti wa Bodi, Hassan O. Kitenge, Mjumbe, Caroline Kanuti, Mjumbe, Nura Mohamed Abubakari, Mjumbe, Matimbila I.Paul, Mjumbe na CPA Poriwoa A. Mbisse. Kwa upande wa Shirika Macrice Mbodo, Postamasta Mkuu pamoja na Menejiment ya Shirika walihudhuria uzinduzi huo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri Jerry Silaa amesema ni vizuri kwa Shirika la Posta Tanzania kuendana na maendeleo ya TEHAMA na mapinduzi ya viwanda ya sasa ili kuimarisha huduma zake na kuchangia zaidi katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.
Aidha ameilekeza bodi kusimamia ubunifu katika huduma za Shirika ikiwemo matumizi bora ya TEHAMA. Pia kutekeleza miradi yenye tija kama vile, mradi wa maghala na duka mtandao. Kuhakikisha ushirikiano thabiti kati ya Bodi Menejimenti na Watumishi ili kuongeza ufanisi.
Waziri Silaa pia amewapongeza Mwenyekiti wa
Bodi, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wote wa Bodi kwa kuteuliwa kwao na amewataka kutumia ujuzi wao wa taaluma mbalimbali
kuhakikisha Shirika linafikia malengo yake.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry William Silaa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika katika makao makuu ya ofisi za Shirika la Posta leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry William Silaa (Mb) pamoja na Viongozi wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na Bodi ya Shirika la Posta Tanzania pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya ofisi za Shirika la Posta leo jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE EMMANUEL MASSAKA WA MICHUZI TV)
No comments:
Post a Comment