HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 11, 2024

UKARABATI MRADI WA MAJI MAKONDE KUGHARIMU SHILINGI BILIONI 84.7

 

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew,akipanda ngazi kwenda kukagua ubora wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6 za maji linalojengwa kupitia mradi wa maji Makonde wilayani Newala.
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew,akigagua ubora wa tenki la maji linalojengwa kupitia mradi wa maji Makonde wilayani Newala, Serikali imetoa kiasi cha Sh.bilioni 84.7 ili kuboresha mradi huo ambao utahudumia wananchi wa Halmashauri ya wilaya Newala, Halmashauri ya Mji Newala,wilaya ya Tandahimba,na Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara.

Na Mwandishi wetu, Newala
NAIBU Waziri wa maji Kundo Mathew,ametembelea na kukagua ukarabati wa mradi wa maji Makonde uliopo wilaya ya Newala mkoani Mtwara unaofanyiwa ukarabati mkubwa na Serikali kupitia wizara ya maji kwa gharama ya Sh.bilioni 84.7.

Mradi huo utakapokamilika utahudumia watu zaidi 670,948 wanaoishi katika Halmashauri ya wilaya Newala,Halmashauri ya mji Newala, wilaya Tandahimba na Halmashauri ya Mji Nanyamba.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo Naibu Waziri Kundo alisema,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imeamua kuwekeza rasilimali fedha nyingi katika sekta ya maji ili kuwaondolea wananchi wa wilaya hizo tatu kero ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama.

Alisema,ukarabati wa mradi wa maji Makonde ulianza tangu mwaka 2022 na ulitakiwa kukamilika mwezi Julai mwaka 2024 lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza Mkandarasi ameomba kuongezewa muda hadi Mwezi Julai 2025.

Alisema, Rais Samia Suluhu Hassan anafuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo kutokana na umuhimu wake na namna anavyowapenda wananchi wa Mtwara, kwa sababu ni mradi wa kimkakati unaokwenda kumaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya hizo.

Alieleza kuwa,mradi utakapokamilika utazalisha lita za maji milioni 26 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya maji kwa miaka 15 ijayo na kuwaomba Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema,wizara ya maji imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi yote ya maji kwa wakati ili wananchi wa wilaya ya Tandahimba,Newala na Halmashauri ya Mji Nanyamba wanaondokana na adha ya kuamka usiku wa manane na kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Mbunge wa Jimbo la Newala vijijini Maimuna Mtanda,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha Wananchi wa wilaya ya Newala kuhusiana na kero ya maji na kutoa Sh.bilioni 84.7 kwa ajili ya kukarabati mradi wa maji wa Makonde.

Alisema,Newala ni wilaya kame,kwa hiyo ujio wa mradi huo ni faraja kubwa kwani utamaliza shida ya maji iliyokuwepo katika wilaya hiyo kwa muda mrefu ambapo wananchi wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo badala yake wanapoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji.

Mtanda,ameiomba Serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika kwenye maeneo yao badala ya kuendelea kukimbizana kwenda kwenye mito na mabonde kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Makonde Francis Bwire alisema,mradi huom ni miongoni mwa miradi minne ya miji 28 inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kwa mujibu wa Bwire,kwa sasa watu wanaopata huduma ya maji safi na salama ni 335,354 sawa na asilimia 62 na kiasi cha maji kinachozalishwa kupitia chanzo cha visima vya Mitema ni wastani wa lita 10,800 kwa siku huku mahitaji ni lita 23,000,000.

Alisema,upungufu wa maji kwa wananchi ni lita 12,200,000 lakini mradi utakapokamilika utakidhi mahitaji ya wananchi wapatao 805,526 kwa kuwa uzalishaji utaongeza kutoka lita 10,800 za sasa hadi lita 36,284 kwa siku ifikapo mwaka 2035.

Rukia Abdala mkazi wa Newala alisema,mradi utakapokamilika utawasaidia kuondokana na kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya ya Newala na wilaya nyingine za jirani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad