Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kimepongezwa kwa kutoa mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini kwa maafisa wanaoshughulikia vitengo husika kwenye majiji, manispaa na halmashauri za Tanzania Bara kwani yanawajengea uwezo watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao. Vitengo hivi ni vipya hivyo mafunzo haya yanakwenda kuimarisha utawala bora kwenye maeneo husika na kusaidia kupanga vipaumbele vya miradi ya maendeleo serikalini.
Afisa Mipango na Uratibu katika jiji la Arusha Ndg. Apolinary Andrew Seiya, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Mh. Mussa Albano Misaile, ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo kwenye ukumbi wa Hazina ndogo katika jiji la Arusha yaliyoanza Oktoba 07, 2024 na yanatarajiwa kumalizika Oktoba 11, 2024.
“Serikali imedhamiria kupeleka huduma bora kwa wananchi ndiyo maana imetumia wataalam bobezi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutoa mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini kwa Maafisa kutoka katika idara za serikali kuu, taasisi na mashirika ya umma pamoja na serikali za mitaa. Haya ni mafunzo ya awamu ya kwanza kwa Maafisa kutoka serikali za mitaa na izingatiwe kuwa serikali za mitaa ziko karibu na wananchi hivyo uboreshaji wa huduma kupitia mafunzo haya ni jambo la muhimu,” amesema Ndg. Seiya.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mkurugenzi wa Kitengo Maalum cha Ushauri wa Kitaamu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dkt. Emmanuel Mallya, amesema mafunzo haya yanalenga kuboresha uwezo wa maafisa mbalimbali wa serikali za mitaa ili kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya miradi, sera na mipango ya serikali kwa lengo la kuimarisha huduma na kuboresha matumizi bora ya rasilimali pesa.
Aidha, Afisa Mipango kutoka jiji la Dar Es Salaam, Bi. Happiness Nchimbi, ameshukuru OWM kwa kushirikiana na OUT kufanikisha mafunzo haya kwa Maafisa Mipango, Wachumi, na Watakwimu na wanaona yana manufaa makubwa kwao kwani yanawaongezea maarifa kwenye usimamizi wa miradi inayoanzishwa hivyo kuwapa ari ya kuwahudumia wananchi na kuzingatia huduma bora.
Mafunzo haya yanafuatia makubaliano kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na ofisi ya Waziri Mkuu yanayolenga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmni kwa taasisi za serikali, mashirika ya umma, serikali kuu na serikali za mitaa za Tanzania Bara. Hii ni awamu ya kwanza ya mafunzo haya, huku awamu ya pili inatarajiwa kufanyika Oktoba 21 hadi Oktoba 25, 2024 jijini Dodoma.
Tuesday, October 8, 2024
Home
Unlabelled
OUT YAENDESHA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI KWA MAAFISA MIPANGO, WACHUMI NA WATAKWIMU SERIKALINI
OUT YAENDESHA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI KWA MAAFISA MIPANGO, WACHUMI NA WATAKWIMU SERIKALINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment