Mhe. Dkt Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba Mbunge wa Viti Maalum aliyeuliza Je, lini Serikali itarudisha mikopo ya asilimia 10 kwa Makundi Maalum.?
Amesema mikopo ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ilisitishwa tarehe 13 Aprili, 2023 ili kupitia na kuboresha utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo kutokana na changamoto zilizobainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka wa Fedha 2021/22.
“Serikali imekwisharekebisha sheria na imeshapitia Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2021 na kutoa Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2024.”
Aidha Dkt. Dugange ameongeza kwa kusema kuwa shughuli zilizoanza kutekelezwa ni kutoa mafunzo kuhusu mfumo mpya wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo kwa wasimamizi 862 katika ngazi ya mikoa na halmashauri. Aidha, mafunzo yanaendelea kutolewa kwa kamati za usimamizi za huduma za mikopo ngazi za kata, halmashauri na wilaya pamoja na vikundi.
“kufuatia mafunzo yaliyotolewa uchambuzi wa awali wa mikopo umeshaanza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na mikopo hiyo inatarajiwa kuanza kutolewa kabla au ifikapo tarehe 30 Novemba, 2024.” Dkt. Dugange.








No comments:
Post a Comment