HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 2, 2024

TAHADHARI KWA WANAOFANYA SHUGHULI ZA KIUCHUMI BAHARINI

 


SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa tahadhari kwa wadau wa usafiri wa majini na wale wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini na kwenye maziwa, kuchukua tahadhari kufuatia taarifa za uwapo wa upepo mkali zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa TASAC, baada ya kupokea taarifa ya uwapo wa upepo huo mkali kutoka TMA, wameona ni vema kuwaeleza wadau wao ili wachukue tahadhari.

Kwa mujibu wa TMA, upepo huo mkali unatarajiwa kuvuma kwa siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 1 hadi Septemba 3 mwaka huu, na unatarajiwa kuvuma kwa kasi inayozidi kilomita 40 kwa saa, na utadhuru maeneo mbalimbali ya pwani ya Bahari ya Hindi na maziwa makuu nchini.

Mamlaka hiyo iliainisha maeneo yenye hatari ya kukumbwa na upepo huo kuwa ni yaliyoainishwa kuwa ni pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini mwa Bahari ya Hindi, hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara, pamoja na baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Ziwa Tanganyika katika mikoa ya Rukwa na Katavi.

Upepo huo pia unatarajiwa kuathiri Ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi, ikihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja, na Pemba. Taarifa hiyo imebainisha kuwa upepo mkali unaweza kuleta athari mbalimbali ikiwemo kuahirishwa kwa shughuli za kiuchumi baharini, kuvurugika kwa ratiba za usafiri wa majini, na hata kuharibika kwa miundombinu ya bandari na maeneo ya karibu.

TASAC imesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau wa sekta ya usafiri na uchumi wa baharini kuchukua tahadhari zote zinazohitajika ili kuepuka ajali na hasara zinazoweza kutokea.

"Wavuvi, wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini, na wale wanaojihusisha na biashara za baharini wanashauriwa kusitisha shughuli zao wakati huu wa tahadhari, mpaka pale TMA itakapotangaza kuwa hali ya hewa imetengemaa."

Taarifa ya TASAC iliwataka wadau wote kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kutoka TMA na kufuata maelekezo yanayotolewa ili kulinda usalama wa maisha na mali na kuahidi kushirikiana na TMA na mamlaka nyingine kuhakikisha kwamba taarifa sahihi na za wakati zinawafikia wadau wote ili kuzuia athari kubwa zinazoweza kusababishwa na upepo huo mkali.

"Kwa kuzingatia hali ya upepo mkali na athari zake, TASAC inawataka wadau wote kuwa makini na kuchukua hatua zinazostahili ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. Hali hii ya upepo mkali ni ukumbusho wa umuhimu wa tahadhari za usalama katika sekta ya usafiri wa majini, hususan katika kipindi hiki ambacho hali ya hewa inabadilika mara kwa mara,"ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad