HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 22, 2024

MWAKIHABA AKEMEA MADEREVA WANAOVUNJA SHERIA BARABARANI WAASWA KUACHA KUTUMIA VILEO

 



Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Edson Mwakihaba, amewataka madereva wa vyombo vya moto kuheshimu alama, michoro ya barabarani na kuacha kutumia vileo kwa ajili ya kutoa uchovu ili kuepusha ajali zembe.


Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 10 ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), Mwakihaba alitoa elimu kwa madereva wa mabasi na pikipiki katika maeneo ya Njuweni na Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mkoani, Wilaya ya Kibaha, kuhusu utii wa sheria za usalama barabarani.


Mwakihaba alisisitiza kuwa kikosi chake hakitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva wanaovunja sheria makusudi.


Aliwapongeza mabalozi wa usalama barabarani kwa jitihada zao za kutoa elimu na kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria, jambo ambalo limechangia kupungua kwa ajali katika Mkoa wa Pwani.


Pia, aliwataka madereva wa mabasi kuwa mfano mzuri kwa kuripoti madereva wengine wanaoendesha kwa mwendo hatarishi, badala ya kusubiri mpaka pale barabara inapofungwa ndipo watoe taarifa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Kanda ya Mashariki, Godfrey Mali, alitoa wito kwa waendesha pikipiki (bodaboda) kuacha kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu au kuchanganya na dawa kama Panadol na Flagyl ili kuondoa uchovu.


Alihimiza kuwa dawa sahihi ya uchovu ni kupumzika.

Aidha, Mali aliwakumbusha waendesha bodaboda umuhimu wa kutumia kofia ngumu, wao na abiria wao, pamoja na kuepuka kupakia abiria zaidi ya mmoja, hali ambayo ni hatari endapo kutatokea ajali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad