Mratibu wa Accelerate Africa Tanzania, Pendo Lema (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano wa Accelerate Africa 2024 utakaofanyika Jijini Arusha Novemba mwaka huu. Wengine kutoka kushoto ni Mratibu wa Maendeleo ya Vijana wa Accelerate Africa, Isaac Fivawo na Katibu Mtendaji Jabeen Shiraz.
*Wajasiriamali zaidi ya 200 kutoka zaidi ya nchi 10 duniani kuhudhuria
Na Mwandishi Wetu.
MKUTANO wa Accelerate Africa 2024 unatarajiwa kufanyika Novemba 28 hadi 29 mwaka huu katika Hoteli ya Gran Melia Jijini Arusha huku ikiwa mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu ambao ni wa tatu baada ya mikutano mingine kufanyika kwa ufanisi mkubwa Rwanda na Afrika Kusini.
Wajasiriamali, wawekezaji na viongozi wa kibiashara zaidi ya 200 kutoka Bara la Afrika watakutana kushirikiana katika kusukuma ukuaji wa biashara ndogo ndogo na za kati (SMEs).
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu wa ‘Accelerate Africa Tanzania’ Pendo Lema, alisema mkutano huo unalenga kuonyesha mitazamo na utaalamu wa aina mbalimbali kutoka sekta za uchumi, ikiwa ni pamoja na sekta ya biashara, teknolojia, na maendeleo.
"Dhamira ya mkutano ni kuwezesha Biashara ndogo ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu na Ubunifu Barani Afrika.'
"Dhamira hii inalenga nafasi ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kukuza ubunifu barani Afrika,” alisema na kuongeza kwamba ‘Accelerate Africa’ ni jumuiya ya washauri mabingwa wa fikira za kiuchumi barani Afrika wanaolenga kufungua ukuaji na ni jukwaa lenye nguvu na ubunifu linalosaidia ukuaji na maendeleo ya biashara ndogo ndogo na za kati katika bara zima la Afrika.
Kulingana na Lema, wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo watajumuisha wajasiriamali, viongozi wa wajasiriamali, watunga sera, na wabunifu kutoka barani Afrika na kwingineko, wote watakaokutanika ili kushirikiana na kubadilishana mawazo na dhamira ya kukuza ujasiriamali, ubunifu, na kuwezesha wafanyabiashara wa ndani kustawi kwenye soko la ushindani la kimataifa.
Alisema wajasiriamali hao watatoka hasa nchi za Botswana, Cameroon, Malawi, Ghana, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Tanzania na Zimbabwe, ambazo ni nchi wanachama wanaounda ‘Accelerate Africa’.
Kuhusu kwa nini Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu Lema alisema, “Tanzania ilichaguliwa kuwa nchi mwenyeji kutokana na eneo lake la kimkakati katika Afrika Mashariki, uchumi wake unaokua kwa kasi, na dhamira yake ya kusaidia biashara ndogo ndogo na za kati na ubunifu. Arusha hasa ni jiji linalotoa mazingira ya kipekee kwa ajili ya kukuza mijadala yenye maana na kujenga mtandao miongoni mwa washiriki.”
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imetangaza ushirikiano wake katika mkutano huo ambao unalenga kuwezesha biashara ndogo ndogo na za kati na kuwa kichocheo kikubwa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.
“Tunajivunia kushirikiana na mkutano wa Accelerate Africa Tanzania 2024 kwani tunatambua umuhimu wa biashara ndogo ndogo za za kati katika ubunifu, kutengeneza ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Kwa kushirikiana na waandaaji, tunalenga kuwapa wajasiriamali nyenzo, rasilimali na mitandao ambayo wanahitaji ili wafanikiwe hapa nchini na barani Afrika,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga.
Alisema kupitia ushiriki katika mkutano huo, TPSF inaimarisha malengo yake katika kukuza ujasiriamali, kuchocea kasi ya ukuaji wa sekta binafsi na kutangaza fursa za boashara na uwekezaji ndani na nje ya Tanzania.
Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa na wazungumzaji na wanajopo ni pamoja na, uongozi na ubunifu, kuwezesha biashara ndogo ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu, ubunifu na upanuzi wa soko, upatikanaji wa fedha na uwekezaji, uwezeshaji wa wanawake na vijana na mageuzi ya kidijitali Afrika.
Zaidi ya hayo, alibainisha kwamba mkutano huo unalenga, miongoni mwa mambo mengine, kukuza ushirikiano na fursa za mtandao kwa biashara ndogo ndogo na za kati barani Afrika, kutoa maarifa muhimu juu ya upanuzi wa soko, uongozi, na ubunifu, kuwezesha kubadilishana maarifa juu ya kufanya biashara endelevu, kuhimiza ubia ambao huchochea ukuaji na maendeleo, akiangazia fursa za uwekezaji na kutoa mwongozo wa vitendo kwa biashara ndogo ndogo na za kati kwa ajili ya ukuaji wake.
Malengo mengine ni pamoja na, kuhimiza Watanzania waishio nje ya nchi kuwekeza katika biashara ndogo ndogo na za kati za Afrika, kukuza uchumi na kuwezesha jamii, kukuza kubadilishana fursa za biashara na mawazo ya ubunifu kati ya wajasiriamali wa Afrika, kukuza ushirikiano na ukuaji na kuwezesha uingizaji na usafirishaji wa bidhaa na huduma kati ya nchi za Afrika na soko la kimataifa na kuimarisha biashara na uchumi barani Africa.
Alisema wajasiriamali wanaweza kujiandikisha kupitia https://accelerateafrica.or.tz/register2.php na kufuata maelekezo ya jinsi wanavyoweza kuhudhuria mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Gran Melia na baadaye kutakuwa na chakula cha jioni ambapo wafanyabiashara bora wadogo wadogo na wa kati 100 watapokea tuzo. "Wafanyabiashara wanaotaka kushiriki katika Tuzo hii wanaweza kijisajili kupitia https://accelerateafrica.or.tz/SmeForm.php," alisema.
Mratibu huyo alitoa wito pia Kwa mashirika mbalimbali ya uma na binafsi wachangamkie fursa hii kudhamini Mkutano huu ili pamoja na mambo mengine watangaze biashara zao, wapate fursa ya kukutana na wadau mbali mbali na pia kufanya biashara.
Tanzania pia itanufaika zaidi kwa vile wajasiriamali watakaohudhuria mkutano huo, wanatarajiwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwa ni pamoja na Ngorongoro, Serengeti na visiwa vya Zanzibar.
Dhamira ya ‘Accelerate Afrika’ ni kuchochea mageuzi ya kiuchumi kwa kutoa rasilimali za kimkakati, ushauri, fursa za kuwa na mtandao, na ufikiaji wa fedha kwa wajasiriamali wanaoibuka. Kupitia mipango yenye matokeo, programu za mafunzo, na ubia shirikishi, jukwaa linalenga kuwa na mfumo mzuri wa ikolojia ambao unakuza na kuharakisha mafanikio ya uanzishaji wa biashara mpya na biashara ndogo ndogo na za kati za Afrika.
No comments:
Post a Comment