Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akiongoza kikao kazi kinacholenga kuanzisha mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni utakaotekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Dodoma, kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao kazi kinacholenga kuanzisha mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni utakaotekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Dodoma, kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Ealiakim Zahabu akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kinacholenga kuanzisha mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni utakaotekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Dodoma, kilichofanyika jijini Dodoma.
MIKOA minne ya Tanzania Bara inatarajia kunufaika na mradi wa nishati safi ya kupikia shuleni ambao utasaidia katika kupunguza matumzi ya kuni na mkaa yanayotokana na ukataji wa miti.
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao kazi kinacholenga kuanzisha mradi wa matumizi ya nisharti safi ya kupikia shuleni kilichoongozwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme jijini Dodoma.
Mradi huo utakaotekelezwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Sustainable Energy for All (SEforALL) unalenga kuwekeza nisharti safi ya kupikia katika shule za mikoa minne ya Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Dodoma.
Aidha, katika mradi huo WFP Tanzania ikishirikiana na Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) inatarajia kufanya uwekezaji wa nishati safi ya kupikia katika shule hizo na baadhi ya kaya nchini.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amewahakikishia wadau wa maendeleo dhamira ya Serikali ya kuunga mkono juhudi hizo.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo hususan katika jitihada hizi zinazochagiza ajenda ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia inayoongozwa na kinara namba moja Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Natambua kazi kubwa inayofanywa na wadau wetu wa maendeleo kwa kushiriki kikamilifu katika uwekezaji huu wa miradi ya nishati safi ya kupikia hapa nchini hususan katika taasisi kama shule ambazo zimekuwa zikitumia kuni nyingi kupikia na hivyo kusababisha ukataji wa miti,” amesema.
Halikadhalika, Bi. Mndeme amesema mradi huo utawapunguzia wanawake safari ndefu na za kuchosha za kukusanya kuni na kuwanyima fursa ya kujishughulisha na shughuli za kutafuta riziki au majukumu muhimu ya utunzaji wa familia pamoja na kuwaweka kwenye unyanyasaji wa kijinsia.
Ameongeza kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kubadilisha nchi kwenda katika nishati safi ya kupikia ambapo umeandaliwa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Kupika (2024-2034), ambao unalenga kubadilisha asilimia ya 80 ya wananchi kutumia nishati hiyo.
Awali akiwasilisha mpango wa mradi huo, Mchambuzi wa masuala ya nishati safi kutoka Shirika la Bw. Jee-Hyun Nam amesema utasaidia kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na katika na kuboresha lishe katika shule.
Pamoja na hayo, pia amesema utasaidia kupunguza utoaji wa kaboni hatua ambayo ni muhimu katika kushughulikia changamoto ya ongezeko la joto duniani.
Bw. Nam amesema kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan katika maeneo yenye watu wengi zikiwemo shule hivyo kupunguza matumizi ya kuni ambazo hutokana na ukataji wa miti.
No comments:
Post a Comment