Sehemu ya kahawa ya magendo iliyokamatwa nyumbani kwa Diwani wa kata ya Mikalanga Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Leons Nombo na kikosi kazi cha kupambana na biashara ya kahawa za magendo ikiwa imeanikwa chini kinyume na taratibu za ubora wa kahawa.
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
KIKOSI kazi cha kupambana na biashara ya kahawa za magendo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,kimemkamata Diwani wa kata ya Mikalanga Halmashauri ya wilaya Mbinga Leons Nombo akiwa na maguni 50 ya kahawa yenye thamani ya Shilingi milioni 35 nyumbani kwake mtaa wa Kiwandani kata ya Mbambi Halmashauri ya Mji Mbinga.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Mbinga Apsa Rashid alisema,kukamatwa kwa Diwani huyo kumetokana na kikosi hicho kuweka mtego baada ya kupata taarifa kwamba kwa muda mrefu Nombo anajihusisha kununua kahawa za magendo kutoka kwa wakulima.
“leo kikosi vya kupambana na biashara ya kahawa za magendo kimefanikiwa kumkamata Diwani Nombo akiwa na magunia 50 ya kahawa ambazo amezipata kwa njia isiyo rasmi ya magoma kinyume na taratibu zilizowekwa zinazowataka wafanyabiashara kununua kahawa mnadani”alisema Rashid.
Ametoa wito kwa wakulima na wafanyabiashara kuzingatia sheria na kufuata taratibu zilizowekwa kuuza na kununua kahawa kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)badala ya kutumia njia ya ujanja ujanja kwani vikosi kazi vipo kazini wakati wote na vinaendelea kufanya msako kwa watu wote wenye nia ya kuvuruga utaratibu uliowekwa na Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Pascal Ndunguru alisema,sheria ya kahawa inawataka wakulima wakishavuna wanatakiwa kupeleka kwenye vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)kabla ya kupelekwa mnadani kwa ajili ya kuuzwa.
“Hapa sisi kama Halmashauri tunajukumu la kuhakikisha kahawa yote ya wakulima inapelekwa kwenye vyama vya msingi vya ushirika ili tuweze kusimamia mapato yanayotokana na ushuru wa zao hilo,sasa kwa hiki alichofanya Mheshimiwa Diwani ni kinyume kabisa na utaratibu na hivyo sheria lazima itumike kudhibiti vitendo vya namna hii”alisema Ndunguru.
Alisema,kahawa iliyokamatwa nyumbani kwa Diwani itapelekwa kiwandani kwa ajili ya kukobolewa ili kupata uzito wake na ile itakayobainika bado haijakauka vizuri itapelekwa kwenye chama cha ushirika na mmiliki ana jukumu ya kufuatilia hadi pale itakapokuwa na sifa ya kupelekwa mnadani.
Alisema,Halmashauri imeunda timu ya mapato yenye jukumu la kufuatilia kuhakikisha wakulima wote wanapeleka kahawa kwenye vyama vya ushirika vilivyoko katika Halmashauri ya wilaya Mbinga ili kujua thamani yake na iweze kupata mapato halali.
Kwa upande wake mdhibiti ubora wa zao la kahawa katika Halmashauri ya wilaya Mbinga Leo Lukenda alisema,mfumo wa kuuza kahawa unatumika kwenye vyama vya msingi vya ushirika ambapo wakulima wanatakiwa kupeleka kahawa zao kwenye vyama hivyo na siyo vinginevyo.
Kwa mujibu wa Lukenda,Diwani huyo licha ya kununua kahawa za wakulima kwa njia ya magendo pia anakiuka utaratibu wa ubora wa kahawa kwa kuanika chini badala ya njia sahihi inayokubalika hali inayopunguza ubora wake.
Amewasisitiza wakulima, kuzingatia suala la usafi na ubora wanaofanya maandalizi ya kahawa ili kuepuka uwezekano wa kupata kahawa yenye ubora mdogo isiyokubalika katika soko la Dunia.
Kwa upande wake Diwani huyo amejitetea kuwa,amelazimika kununua kahawa hiyo baada ya kufuatwa na wakulima wenyewe ili waweze kupata fedha za haraka kwani hawawezi kusubiri hadi mnada utakapofanyika kutokana na changamoto walizonazo.
Diwani wa kata ya Mikalanga Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Leons Nombo wa tatu kulia,akionyesha sehemu ya kahawa ya magendo iliyokutwa nyumbani kwake mtaa wa kiwandani kata ya Kipika Halmashauri ya Mji Mbinga baada ya kikosi kazi cha kupambana na biashara ya kahawa ya magendo wilayani humo kufika nyumbani kwa Diwani huyo majira ya saa sita usiku ambapo jumla ya magunia 50 yenye thamani ya Sh.milioni 35 yalikamatwa.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbinga SSP William Mwamafupa kushoto,akimsikiliza Diwani wa kata ya Mikalanga Halmashauri ya wilaya Mbinga Leons Nombo aliyekutwa na magunia 50 ya kahawa za magendo nyumbani kwake mtaa wa kiwandani kata ya Kipika baada ya kukamatwa na kikosi kazi za kupambana na biashara ya kahawa ya magendo kilichoundwa na Mkuu wa wilaya hiyo Kisare Makori.
No comments:
Post a Comment