Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania na China leo zimesaini Itifaki ya kuuza Asali ya Tanzania nchini China huku Serikali ya Tanzania ikitoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa ya kuzalisha asali yenye ubora kwa wingi ili kuinua vipato vyao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Soko la China lina zaidi ya watu bilioni 1.4 na linaagiza nje ya nchi zaidi ya tani za asali milioni 38 kwa mwaka.
Utiaji saini umefanyika leo Agosti 15,2024 jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa Tanzania umefanywa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula na upande wa China Waziri na Katibu wa Kamati ya CPC ya Utawala wa Forodha ya Watu wa China Yu Jianhua
Akizungumza na vyombo vya habari, mara baada ya utiaji saini huo Mhe. Kitandula ameeleza kwamba mkataba huo sasa unaondoa kikwazo kilichokuwepo hapo awali na kukidhi haja ya wafanyabiashara wa Tanzania ya kuuza asali katika masoko ya China.
Aidha, amesema kufunguka kwa soko la asali nchini China kunaenda pamoja na kutekeleza masharti kadhaa yaliyobainishwa kwenye Itifaki.
“Moja ya sharti ambalo wafanyabiashara wenye nia ya kuuza asali nchini China, nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani wanapaswa kutekeleza ni kuhakikisha kuwa Kampuni zao zinasajiliwa kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na Usalama wa Vyakula; Afya ya Mimiea; na Ulinzi wa Mazingira”. Amesisitiza
Amefafanua kuwa usajili wa Wafanyabiashara/Makampuni katika Mifumo hii hufanyika kwa njia ya kidigitali na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambako kuna dawati maalum kwa ajili ya kusaidia Wafanyabiashara kujisajili na kutoa rai kwa Makampuni ambayo bado hayajasajiliwa yasajiliwe.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya Serikali katika kusaidia wananchi wanaofanya biashara hiyo amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji nyuki na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki kwa kutoa Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazohusiana na ufugaji nyuki na kuongeza thamani mazao ya nyuki.
Pia amesema Serikali imejenga viwanda sita vya kuchakata mazao ya nyuki katika Wilaya za Kibondo, Sikonge, Mlele, Nzega, na Bukombe ili kuhakikisha kuwa asali inayouzwa nje ya nchi inakuwa na viwango vya ubora vinavyokidhi mahitaji ya masoko hayo.
Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 138,000 za asali kwa mwaka. Hata hivyo, kwa sasa uzalishaji wa asali upo kwenye kiwango cha takribani tani 33,276 sawa na asilimia 24.1 ya uwezo uliopo.
Kiwango hiki kinaiweka Tanzania katika ramani ya Dunia na kuifanya kuwa nchi ya Kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki na SADC; nchi ya Pili kwa uzalisahji wa asali barani Afrika; na nchi ya 14 Duniani kwa uzalisahji wa asali.
Hii inaonyesha kuwa sekta ya ufugaji nyuki ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na ina nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na ajira kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment