HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 5, 2024

SERIKALI KUMWAGA A AJIRA 37, 616 - NAIBU WAZIRI MHE. SANGU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza leo na wananchi wa Kijiji cha Laela , Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa , ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akisalimiana na wananchi mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Laela , Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa , ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Lusaka, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Kitete, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.


Na. Lusungu Helela-Rukwa
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema Serikali imepanga kutangaza jumla ya ajira mpya 37, 616 huku ajira za kada ya Ualimu, Afya na kada nyinginezo ikiwemo kada ya uhasibu na ugavi zikiwa tayari zinaendelea kutangazwa lengo likiwa ni kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi nchini.

Mhe. Sangu ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Kitete, Laela, Kamsamba na Kavifuti vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipouteliwa kushika wadhifa huo.

Akizungumzia nafasi za ajira ya ualimu ambazo tayari zimeshatangazwa na Sekretarieti ya Ajira kwenye ngazi ya mikoa kulingana na mahitaji ya mkoa husika, Mhe. Sangu amesema utaratibu wa kuwapata walimu kwa mwaka huu umeanza kuwa wa tofauti ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Amefafanua kuwa usaili huo umeanza kufanyika kwa kada ya ualimu kwa sababu nafasi za ajira za ualimu ni chache ukilinganisha na idadi ya walimu wa shule ya msingi na sekondari waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini ambapo zaidi ya walimu100,000 wapo mtaani wakiwa hawana ajira.

Amesema Serikali imekuja na uamuzi huo ili kuchagiza dhana ya ushindani kwa lengo la kuhakikisha kila mwenye sifa stahiki anapata ajira katika mazingira aliyopo pasipo kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya usaili.

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Sangu ametoa wito kwa vijana waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini kuchangamkia nafasi hizo za ajira huku akiwataka wajiandae ipasavyo kwa ajili ya usaili huo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kada hiyo ya ualimu kufanya usaili

Ametumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wote walioomba nafasi hizo za ualimu huku akiwahakikishia kuwa Ofisi yake yenye dhamana ya kusimamia masuala ya ajira nchini imejizatiti kuhakikisha mchakato huo wa kuwapata walimu wenye sifa stahiki utakuwa wa huru na haki.

“Katika kumsaidia Waziri wangu Mhe, George Simbachawene tutahakikisha sera ya ajira nchini inayosisitiza haki ya kupata ajira bila kujali hali ya kiuchumi, rangi, kabila na dini inazingatiwa kikamilifu.” Mhe. Sangu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad