Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM wa Mkoa wa Dodoma katika Mkutano uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete tarehe 16 Agosti 2024.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Serikali ngazi ya Mkoa wa Dodoma kuendelea kutafutia ufumbuzi migogoro ya ardhi iliyokithiri hususan fidia kwa ardhi iliyotwaliwa na utekelezaji wa mgawanyo wa ardhi wa 70% kwa 30%.
Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma katika Mkutano uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema changamoto hiyo ya ardhi mkoani Dodoma kwa kiasi kikubwa imewafanya wanachama pamoja na wananchi kuwa na manung’uniko na hata kufikia hatua ya kususia uchaguzi. Amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kushirikiana na Waziri wa Ardhi kwa pamoja na uongozi wa Jiji la Dodoma kuongeza nguvu zaidi katika kushughulikia migogoro hiyo.
Mheshimiwa Dkt. Mpango amewahimiza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Dodoma kusimamia miradi na mapato ya Chama kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mali za CCM zinatumika kwa manufaa ya Chama ili kuimarisha uchumi na kuepuka kuathiri uendeshaji wa shughuli za Chama hicho. Aidha amewasihi kusimamia vema na kuhimiza ulipaji wa ada za uanachama suala ambalo ni muhimu na la kikatiba.
Makamu wa Rais amewataka wanachama na viongozi wa CCM mkoani Dodoma kuhakikisha hali ya utulivu inakuwepo katika chama kwa kuendelea kutekeleza vema majukumu katika ngazi zote, kufuata Kanuni na Taratibu zote, kufanya vikao kwa kuzingatia Katiba ya Chama na kalenda ya vikao, kuondosha mivutano yoyote baina ya Viongozi au Viongozi na Wanachama inayotishia ustawi wa Chama hicho.
Halikadhalika amewaagiza viongozi na wanachama kuepuka siasa za makundi na migogoro ndani ya chama. Amesema ni muhimu kufanya maamuzi yahusuyo chama kupitia vikao halali na kuwasihi kufanya vikao katika ngazi za mashina, matawi, kata, Wilaya na Mkoa pamoja na kuendesha semina za mafunzo ya itikadi ya chama.
Pia ametoa rai kwa viongozi wa CCM wa ngazi zote kudumisha ushirikiano na kuendeleza uhusiano mzuri wa kikazi na Watendaji wa Serikali kwa kufanya kazi kwa karibu ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 kwa kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais na Mlezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa amesema Chama cha Mapinduzi mkoani humo kimeendelea kujiweka karibu na wananchi kwa kusikiliza na kutatua kero zao ambapo katika changamoto ya migogoro ya ardhi kwa kipindi cha mwezi Januari – Julai 2024 jumla ya watu 674 walitatuliwa migogoro yao na chama hicho.
Kimbisa ameongeza kwamba Chama kimeendelea kutoa mafunzo ya itikadi, kuhamasisha ulipaji wa ada za wanachama pamoja na kuingiza wanachama wapya kwa kuwasajili katika mfumo wa kielekrotiniki.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema mkoa huo umeendelea kutatua kero mbalimbali za wananchi ambao kwa kipindi cha miaka mitatu jumla ya kero zaidi ya 26,000 zimetatulia huku kero zaidi ya 4000 zikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi. Amesema kwa sasa mkoa huo umeingia katika mfumo maalum kutoka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora unaowawezesha wananchi wa Mkoa wa Dodoma wanauwezo wa kutuma kero zao katika mfumo huo na kutatuliwa.
Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi kutoka kata 209 za mkoa wa Dodoma, Wabunge, Madiwani, Machifu, Wazee wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Wanachama.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
16 Agosti 2024
Dodoma.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa CCM, Wazee na Machifu wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kuzungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM wa Mkoa wa Dodoma katika Mkutano uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete tarehe 16 Agosti 2024.
No comments:
Post a Comment