Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametoa maelekezo kwa mawaziri wanne kufuatia maombi ya wananchi wa Mwandiga, mkoani Kigoma kuhusu umeme, usalama wa raia na mali zao, maji na kituo cha afya.
Balozi Nchimbi ambaye yuko Kigoma akiendelea na ziara yake ya siku 3 mkoani humo, aliyoanza Agosti 4, 2024, ametoa maelekezo kwa wizara hizo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mwandiga, Jimbo la Kigoma Kaskazini, aliposimama kuwasalimia akiwa njiani kuelekea Wilaya ya Kasulu.
Maelekezo ya kwanza ya Balozi Nchimbi yalielekezwa kwa Waziri wa Nishati, akiitaka wizara hiyo iongeze kasi katika kusambaza umeme kwenye ngazi ya vitongoji baada ya kumaliza vijiji vyote nchini.
Aidha, Balozi Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhakikisha kinajengwa kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao eneo la Mwandiga na maeneo mengine ya jirani jimboni humo, ambapo walionesha uhitaji huo kupitia mabango yao wakati wakimpokea Katibu Mkuu huyo wa CCM, pia kutokana na maombi ya mbunge wao, Mhe. Assa Makanika alipokuwa akizungumzia maendele ya jimbo hilo kwenye mkutano huo.
“Wakati naingia hapa nimeona mabango, watu wangu wasaidizi wameyachukua kuyafanyia kazi. Mojawapo ya bango limenifurahisha sana, limesema mnahitaji kituo cha polisi. Imenipatia furaha kwamba ninyi ni watu wema sana. Watu wabaya, majambazi, wezi au wakabaji au wabakaji hawawezi kuomba kituo cha polisi.
“Namwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ahakikishe Kituo cha Polisi kinajengwa hapa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Sasa RC (Mkuu wa Mkoa wa Kigoma) kwa kushirikiana na Waziri, wananchi wajengewe kituo cha polisi hapa,” amesema Katibu Mkuu Balozi Nchimbi.
Vile vile, Katibu Mkuu wa CCM alitoa maelekezo kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), aliyewakilishwa na Naibu Waziri Mhe. Zainabu Katimba, akimwelekeza afikishe maelekezo hayo kwa Waziri, kuhusu mahitaji ya kujengwa kwa Kituo cha Afya kwa ajili ya Tarafa ya Mwandiga.
“Mhe. Naibu Waziri nakuongeza kwa maelezo yako mazuri sana. Hili la kituo cha afya umelisemea vizuri tayari. Lakini maelekezo hapa ni kwamba habari za mchakato zimeisha, wananchi hawa wajengewe kituo cha afya kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Naomba utufikishie kwa Mhe. Waziri ambaye pia ni mtu mchapakazi mzuri.”
Maelekezo mengine ya Katibu Mkuu Balozi Nchimbi aliyaelekeza kwa Wizara ya Maji, kutokana na wananchi kumpatia taarifa kuwa mtandao wa maji hautoshelezi mahitaji kulingana na idadi ya watu katika eneo hilo la Mji Mdogo wa Mwandiga.
“Waziri wa Maji atatakiwa kuja huku kwa haraka afanyie kazi suala hili. Na akifika huku Kigoma apite hapa Mwandiga pia kuangalia ufumbuzi wa suala hili la mtandao wa maji maeneo haya ili tumalize hii changamoto huku Kigoma Kaskazini,” amesema Katibu Mkuu Balozi Nchimbi, ambapo pia aliwapongeza mawaziri wote hao aliowapatia maelekezo kuwa ni watu wachapakazi, wanaojua mahitaji ya wananchi na kutekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025.
Monday, August 5, 2024
Home
Unlabelled
DK NCHIMBI NA MAAGIZO KWA MAWAZIRI HAWA, KIGOMA
DK NCHIMBI NA MAAGIZO KWA MAWAZIRI HAWA, KIGOMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment