Na WAF - Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kujengwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kuanza ujenzi wa jengo la Afya ya uzazi mama na mtoto ili kurahisha upatikanaji wa huduma hizo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo Agosti 6, 2024 akiongea na wananchi wa mkoa wa Morogoro wakati akihitimisha ziara yake mkoani humo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha 'Serengeti Cigarette Company' (SCC) pamoja na kuzindua jengo le Maabara jumuishi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.
"Nataka nikubaliane nanyi kwamba sasa, Hospitali tuliyonayo haikidhi vigezo vya kuwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa kwa ulimwengu wa leo, hivyo basi nimempa maelekezo Waziri wa Afya apate Bilioni 5 za kuanzia ujenzi wa Hospitali ya Rufaa." Amesema Rais Samia
Amesema, Hospitali hiyo itaanza kujengwa majengo makubwa ya mama na mtoto zikiwa na vifaa vyote vya kutolea huduma hizo ikiwemo vyumba vya upasuaji pamoja na wodi ya uangalizi maalum (ICU), kisha kufuatia wodi nyingine hadi kukamilika kwa Hospitali hiyo.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imejenga vituo vya Afya 136 ili kurahisha huduma za Afya ikiwemo huduma za mama na mtoto katika mkoa wa Morogoro.
"Vituo hivi vinasaidia sana lakini lile ombi la Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini Mhe. Abdul-Aziz Abood la kuwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya kisasa tunakwenda kulitekeleza." Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
No comments:
Post a Comment